Dc Moshi: Teknolojia itumike kukabili mabadiliko tabia nchi

 Wasimamizi wa vivutio vya utalii nchini wametakiwa kutatua changamoto za migogoro na tabia ya nchi kwa njia ya maridhiano ikiwa ni pamoja na kuwekeza kwenye teknolojia ili kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazoyakabili maeneo hayo.

Rai hiyo imetolewa Mei 5, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya urithi wa dunia barani Africa, yaliofanyika Kitaifa wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro (Kinapa) ambayo ni miongoni mwa maeneo saba ya urithi wa Dunia nchini.

Makori amesema maeneo mengi ya urithi wa dunia, yanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo zile zinazochangiwa na shughuli za kibinadamu na badhi ya changamoto hizo ni mabadiliko ya tabianchi, vitendo vya ugaidi, uwindaji haramu, kupanuka kwa ujenzi wa makazi kusikosimamiwa vizuri na kukosekana kwa mipango mzuri.


Aidha amesema kwa sasa teknolojia inakua kwa kasi duniani hivyo ipo haja ya kuwekeza kwenye teknolojia ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika maeneo ya urithi wa dunia ikiwemo ya uwindaji haramu.

"Nitoe rai kwa mameneja wa maeneo ya urithi wa Dunia, kufanya shughuli yenu kwa usahihi kwani mmepewa dhamana hiyo kwa niaba ya Serikali hivyo tekelezeni majukumu yenu ili kuulinda urithi wa Dunia,"amesema.

Katika hatua nyingine, Makori amewataka wataalamu na wadau wa utalii nchini, kufanya tathimini juu ya maeneo mengine yanayofaa kuingizwa kwenye uridhi wa Dunia na kuandika maandiko ili yaweze kuingizwa, hatua ambayo itachochea ukuaji wa kipato na kuongeza idadi ya watalii nchini.

Ofisa mhifadhi mkuu wa Kinapa, Dk Iman Kikoti amesema bado zinahitajika jitihada za pamoja duniani kuhakikisha maeneo ya urithi wa dunia yanalindwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kukabiliana na changamoto zinazoyakabili maeneo hayo.


"Hatari kubwa ambayo imeyakumba maeneo ya urithi wa dunia nchini ni mabadiliko ya tabianchi ambayo yameleta madhara makubwa, shughuli za kibinadamu na uvamizi katika hayo maeneo, hivyo wadau tunahitajika kukaa pamoja ili kutafuta suluhisho la changamoto hizi kwa maslahi mapana ya Taifa,"amesema.

Akizungumza  kwa niaba ya Kamishina wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Emiliani kiwele amesema  ni jukumu la kila mwananchi kuhakisha anavilinda,anavitunza na kuendeleza vivutio vilivyopo nchini ikiwemo vilivyopo kwenye urithi wa dunia ili visitolewe kwenye sifa hiyo.

Naye, Ofisa Utamaduni wa Shiraka la Umoja wa Mataifa linalohusiana na Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), Nancy Mwaisaka amesema siku ya urithi wa Dunia Afrika ni fursa kwa watu wote duniani hususan Afrika katika kusherekea urithi pekee wa kitamaduni na asili uliopo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments