Shughuli ya uzinduzi huo ilianza alfajiri kwa wageni mbalimbali kuanza kuwasili katika viwanja vya Ikulu mpya huku wageni mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Rais Samia aliwasili saa 4:15 asubuhi na kupokelewa na makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein mwinyi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na viongozi wastaafu akiwemo Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete.
Bada ya kupokelewa, Rais Samia alikwenda katika jukwaa lililoandaliwa kwa ajili ya kupokea heshima ya kijeshi. Baada ya heshima hiyo, Rais Samia alikagua gwaride lililoandaliwa maalumu kwa shughuli hiyo.
Rais Samia alikwenda kupanda mti wa kumbukumbu ulio mbele ya jengo la Ikulu ya Chamwino ambalo lilianza kujengwa mwaka 2020 na kukamilika miezi 30 baadaye.
Baada ya hatua hiyo, Rais Samia na viongozi wengine walisimama mbele ya jengo la Ikulu kushuhudia bendera zikipandishwa juu ya mnara wa jengo hilo huku baragumu likipigwa. Bendera tatu zilipandishwa ambazo ni bendera ya Rais, bendera ya Taifa na bendera ya Afrika Mashariki.
Rais Samia na makamu wake walielekea kwenye lango kuu la kuingia ndani ya Ikulu na kupiga ngoma zilizokuwa zimewekwa hapo ikiwa ni ishara ya ufunguzi huo. Baada ya hatua hiyo, Rais Samia aliingia ndani kukagua jengo lanyewe.
Viongozi walimaliza ukaguzi huo na kuelekea kwenye jukwaa kuu ambako walikuwa wakisubiriwa na wageni mbalimbali walioalikwa kushuhudia historia mpya ikiandikwa kwa Ikulu iliyojengwa na wazawa, Suma JKT pamoja na Wakala wa Ujenzi (TBA).
0 Comments