Taarifa kutoka ndani ya familia zinasema taa ya Membe ilizimika ghafla asubuhi ya leo Ijumaa, Mei 12; katika Hospital ya Kairuki (HK) iliyoko Mikocheni, jijini Dar es Salaam, akiwa anapatiwa matibabu, baada ya kupelekwa mapema leo kutokana na changamoto ya homa na kifua.
Membe ambaye anatajwa kama Kachero mbobevu, Mwanadiplomasia nguli na Mwanansiasa makini, aliwahi kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu 2020, akipeperusha bendera ya ACT Wazalendo.
Kuzaliwa
Historia ya Mwanadiplomasia huyo imeanzia katika Kijiji cha, Rondo, Chiponda, Wilaya ya Lindi Vijijini, ambapo Novemba 9, 1953; katika familia ya mwindaji Kamillius Anton Ntanchile na mkewe Cecilia John Membe, walibahatika kupata mtoto wao wa pili, japo baadaye walizaliwa wengine watano na kuifanya familia kuwa na jumla ya watoto saba.
Waziri huyo wa zamani ni Mmwera, na kama ilivyo desturi ya watu wa kabila hilo, watoto hutumia jina la ukoo wa Mama, na hii ndiyo sababu Bernard na ndugu zake, wamekuwa wanatumia jina la ubini la upande wa mama yao Cecilia, yaani Membe.
Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa vya habari, baba yake Membe alitamani kazi ya uwindandaji toka akiwa na miaka mitano, na hii ilitokana na ukweli kuwa, alimshuhudia Simba akimkamata na kumrarua mama yake, na hivyo kujiapiza kuwa, akiwa mkubwa atamiliki bunduki na kuwa mwindaji, jambo ambalo alifafanikisha.
Mzee huyu (Baba yake Membe) alifariki dunia mwaka 1987 kwa kuvuja damu nyingi kutokana na kuchelewa kupata msaada wa kitabibu kwa zaidi ya saa 10, baada ya kulipuliwa na bunduki akiwa katika harakati zake za uwindaji.
Elimu
Membe alianza elimu ya msingi akiwa na miaka tisa, katika Shule ya Msingi Rondo-Chiponda (1962-1968). Akiwa na shauku ya kuhudumu kama mtumishi wa kanisa (Padri), alijiunga na masomo ya sekondari katika seminari ya Namupa (1969-1972), baadaye kuendelea Itaga Seminari iliyopo Tabora, kwa masomo ya kidato cha tano na sita (1973-1974).
Mafunzo na Kazi
Kati ya mwaka 1975 na 1976 Membe alijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kambi ya Oljoro, Arusha. Hii ni ilikuwa ni kwa mujibu wa Sheria ambapo vijana wote waliohitimu kidato cha sita walitakiwa kujiunga na mafunzo ya Jeshi kwa muda wa mwaka mmoja.
Na kutokana na uwepo wa Azimio la Musoma lililotaka watu wote waliomaliza kidato cha sita kufanya kazi miaka miwili kabla ya kujiunga na masomo ya chuo kikuu, baada ya mafunzo ta JKT, Membe hakurudi tena kuendelea na masomo yake ya upadri, kazi aliyotarajia kuifanya, badala yake aliajiriwa katika Ofisi ya Rais, Utawala Bora.
Akiwa kazini, 1978, alifanikiwa kupata mafunzo ya sheria za Jinai na Usalama wa nchi, nchini Uingereza. Miaka miwili baadaye, alipata mafunzo ya siasa, katika chuo cha Kivukoni kilichokuwa kikimilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, Membe alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) mwaka 1981/82 akisomea digrii ya awali ya Sayansi ya Siasa na Mahusiano ya Kimataifa. Matokeo yake katika chuo hicho, yanaonyesha kwamba Membe alifaulu vizuri kwa kiwango cha kupata GPA ya 4.1.
Kutokana na ufaulu huu, angeweza kuajiriwa kuwa mwalimu wa chuo kikuu, na taarifa zinaonyesha kwamba alipewa barua ya ajira ya uhadhiri pale Udsm katika ngazi ya uhadhiri msaidizi (tutorial assistant).
Hata hivyo, hakuweza kujiunga na chuo hicho kwani mwajiri wake alimtaka kurudi kazini mara baada ya kumaliza masomo yake.
Hivyo alirudi serikalini kuendelea na ajira yake katika Ofisi ya Rais, ambapo taarifa zinaweka wazi kuwa kwa kuwa alikuwa na shauku ya kusoma, 1992; alitunikiwa digrii ya pili (Masters) katika Uchumi, Mahusiano ya Kimataifa na Sheria za Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, kilichopo Washington DC, Marekani, moja ya vyuo bora kabisa duniani.
Famila
Mwaka 1986, Membe alifunga ndoa takatifu na Dorcas Richard Masanche, katika Parokia ya Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam. Membe na mkewe walijaaliwa kupata watoto watatu, ambao ni Cecilia, Richard na Denis.
Siasa
Mwanadiplomasia huyu ametumikia nafasi mbalimbali ikiwemo Kamanda wa Vijana CCM wa Mkoa wa Lindi, Mjumbe wa Kamati Kuu, na Katibu wa Secretarieti ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa chama hicho.
Mwaka 2000, aliingia Bungeni baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo la Mtama, na michango yake ilijikita sana katika mijadala inayohusu Amani, Ulinzi na Usalama lakini pia mambo yahusiyo Utawala Bora.
Mwaka 2005, alichaguliwa tena kuwa Mbunge wa jimbo hilo, na January 2006, Membe alianza kutumika kama Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani baada ya kuteuliwa na Rais Kikwete.
Hata hivyo, kufuatia mabadiliko ya Baraza la Mawaziri mwezi Oktoba, 2006, Bernard Membe alihamishwa wizara na kuwa Naibu Waziri Nishati na Madini, moja ya wizara inayoelezwa kuwa ngumu na nyeti kwa Taifa.
Aidha, miezi michache baadae, (January 2007), Rais Kikwete alimteua Membe kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, baada ya aliyekuwa anashikilia wadhifa huo Dr Asha Rose Migiro, kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN).
Membe amehudumu katika nafasi hiyo kwa miaka nane mfululizo na hivyo kuwa Mtanzania wa pili kushika wadhifa huo mda mrefu , akitanguliwa na Rais Kikwete ambaye alidumu katika Wizara hiyo kwa miaka 10 mfululizo.
Mafanikio
Wadadisi wa mambo wanasema chini ya uongozi wa Membe katika Wizara ya mambo ya Nje na Uhsirikiano wa Kimataifa, Tanzania iliendelea kuwa mtetezi na mshirika mkubwa wa ulinzi na usalama ndani ya Ukanda wa Afrika na duniani.
Aidha, Tanzania imeshiriki kuleta amani katika nchi za Maziwa makuu yaani, DRC, Burundi na Malawi, lakini pia Tanzania imeshiriki katika utatuzi wa migogoro ya kisiasa katika nchi za Comoro, Madagasca, na Sudan ya Kusini.
Pia Tanzania imekuwa mshiriki mzuri katika kuchangia vikosi vya kulinda amani katika mataifa ambayo yalipata machafuko kisiasa.
Hata hivyo, toka 2006, Membe alifanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali, zikiwemo Mwenyekiti Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Afrika, Mkuu wa Waangalizi wa Uchaguzi Mkuu Zimbabwe kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc), na Mwenyekiti Baraza la Mwaziri wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth).
Katika kipindi cha Membe kama Waziri ashughulikaye na mambo ya nje, Tanzania ilitembelewa na viongozi mbalimbali mashuhuri wengi, baadhi ya ni Marais George W. Bush na Baraka Obama wote wa Marekani, Xi Jinping wa China, na Joachim Gauck wa Ujerumani.
Vilevile, Tanzania ilipanua wigo wa mahusiano yake Kaimataifa kwa kufunguwa Balozi mpya katika nchi za Malaysia, Brazil, Comoro, Oman, Umoja wa Falme za Kiarabu na Kuwait.
Aidha, Wizara ilifanikiwa kufungua upya Ubalozi wa Tanzania the Hague, Uholanzi uliofungwa mwaka 1994. Kadhalika Balozi Mpya za Brazil, Oman, Uturuki, Kuwait, Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Namibia zilifunguliwa hapa nchini.
Membe ataendelea kukumbukwa kwa mchango wake katika kurejesha hali ya amani na utulivu katika Visiwa vya Comoro, mwaka 2008, kwani alikuwa miongoni mwa watanzania waliotunukiwa Nishani ya Operesheni Demokrasia Comoro na rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Kutoka na Kurejea CCM
Membe alijiunga na ACT Wazalendo Julai 15, 2020 akisema katiba ya chama hicho na itikadi yake ya kutaka kuleta mabadiliko ndivyo vilivyomvutia. Aligombea Urais wa Tanzania kupitia chama hicho na kibuka na kura 81,129 sawa na asilima 0.5 ya kura zote.
Oktoba 5, 2022 mbele ya Waziri Mkuu Kasim Majaliwa, Jasusi huyu alieleza kuunga mkono utendaji wa Rasi Samia Suluhu Hassan huku akichombeza kuwa yuko njiani kurejea nyumbani.
Machi 31, 2022 CCM ilitangaza kumpokea na kumrejeshea uanachama wake, baada Kamati Kuu ya chama hicho chini ya uongozi wa Hayati John Magufuli, kuazimia kwa kauli moja na kumfukuzwa uanachama kwa kile kilichoelezwa "amekuwa na na mwenendo usiofaa."
Kifo Chake
Kwa mujibu wa daktari wake binafsi, Profesa Harun Nyagori; kifo cha mwanasiasa huyo kimesababishwa na ugonjwa wa maambukizi ya mfumo wa mapafu hewa, ambao unasababisha mgando wa damu na kuzuia mapafu kupeleka hewa ya oksijeni.
Raha ya Milele umpe ee Bwana, na mwanga wa milele umwangazie; apumzike kwa Amani.
Makala hii imeandikwa kwa msaada wa vyanzo mbali mbali.
0 Comments