Mitaa yote ya Kariakoo imeonekana kurejea kwenye uhai wake huku wafanyabiashara hao wakifungua maduka yao kama ilivyo ada ya soko hilo, huku wakieleza juu ya imani waliyo nayo kwa Kiongozi huyo namba tatu nchini.
Jana Jumatano Mei 17, Waziri Mkuu Majaliwa aliunda tume ya watu 14 ambayo itachakata kero na mapendekezo ya wafanyabiashara wa soko hilo la Kimataifa la Kariakoo na hivyo kufikia tamati ya kero zilizosababisha kufunga biashara zao.
Wakati wafanyabiashara hao wakifungua maduka na kuendelea na shughuli zao, pia wameeleza kuwa na imani na kamati hiyo ambayo itafanya kazi kwa wiki mbili, na kupeleka mapendezo yatakayokuwa suluhisho la malalamiko yaliyoibuliwa na wafanyabiashara hao.
Wafanyabiashara hao waliitishata mgomo kwa siku tatu tangu Mei 15 kutokana na changamoto mbalimbali zilizilokuwa zinawakabili zikiwemo za kikodi.
Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Mei 18, 2023 baadhi yao, wakiwemo wale wanaouza vitenge; wamemshukuru Waziri Mkuu Majaliwa kuunda kamati hiyo.
"Hasa sisi wafanyabiahara wa vitenge tangu mwaka 2019 tumeshindwa kufanya biashara kutokana na kupandishiwa kodi kitendo kilichofanya tukashindwa kuagiza," Richard Ndanshao ambaye ni mfaanyabiashara wa vitenge sokoni hapo.
Alisema Mkutano baina ya Serikali na wafanyabiashara umeibua mambo mengi ambayo hata wao walikuwa hawajui, hivyo kamati hiyo itaenda kufungua mwanga kwenye biashara zao.
Mfanyabiashara mwingine Anna maarufu mama Mkapa amesema kitendo cha wafanyabiashara kufungua, imeonyesjmha ni namna gani serikali ina nia ya kutatua changamoto zinazowakabili.
"Kwa upande wangu mimi nilishakata tamaa na biashara, nalipa kodi ya bure hata ningefunga wiki sioni hasara, lakini kwa kauli hii ya serikali tunauhakika wa kufanyika mabadiliko," alisema Anna.
0 Comments