Karume aonya makundi CCM, serikalini

Mwanasiasa na mwanadiplomasia, Balozi Ali Karume ameonya kuendelea kuwapo kwa makundi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali, akisema endapo chama hicho kitashindwa uchaguzi Zanzibar, kitachukua muda mrefu kurudi madarakani.

Kauli ya Balozi Karume imekuja wakati hivi karibuni Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alikiri kuwapo kwa makundi hayo ndani ya chama, alipokuwa akiwahutubia viongozi na watendaji wa chama, katika ziara yake Mkoa wa Mjini Magharibi.

“Ningependa kusema chagamoto moja ambayo kwa kiwango kikubwa inaathiri sana utendaji wa Serikali yetu na chama, ni kwamba bado kuna makundi ndani ya uongozi. Ombi langu kama nilivyosema awali uchaguzi umekwisha sasa ivi tuwe kitu kimoja, tujitahidi kuondoa makundi, maana makundi ndiyo yanayoathiri chama hiki,” alisema Rais Mwinyi.


Alichosema Balozi Karume

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti la The Citizen nyumbani kwake Maisara mjini hapa mwanzoni mwa wiki hii, Balozi Karume alisema uchaguzi wa Zanzibar una tofauti ndogo ya matokeo na kwamba makundi yana madhara makubwa kwa uhai wa chama.

Alisema kama chama hakitachukua hatua ya kuondosha makundi hayo na kujenga umoja na mshikamano na kusimamia misingi ya mapinduzi na muungano, kinaweza kupoteza uchaguzi.

Alisema kwamba makundi yaliyojitokeza ndani ya CCM yametokana na mfumo uliotumika wa kumpata mgombea urais wa Zanzibar mwaka 2020, kwa sababu ilikuwa kwa njia ya uteuzi badala ya uchaguzi katika vikao vya chama.

“Utaratibu uliozoeleka ndani ya chama haukufuatwa, badala yake watu waliteuliwa bila kujali kama wana sifa zinazohitajika,” alisema balozi huyo.

Aidha, Balozi Karume alisema ndani ya CCM kuna kiongozi mmoja amekuwa akitoa maneno ya kejeli na kuwadharau viongozi wastaafu bila kuheshimu mchango wao katika kuitumikia Serikali ya Zanzibar na Tanzania.


‘‘Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni bila kuvunja sheria, lakini kwa bahati mbaya kuna mtendaji mmoja mkuu wa chama anashindwa kuheshimu uhuru wa kikatiba wa watu kutoa maoni yao na kuwashambulia watu, wakiwemo viongozi wastaafu bila kujali mchango wao walioutumikia katika Taifa,’’ alisema.

Kulingana na Balozi Karume, ambaye amewahi kuwania tiketi ya kugombea urais wa Zanzibar na Muungano kupitia CCM, ndani ya chama hicho kuna utaratibu uliozoeleka kwamba kiongozi anapochaguliwa, inapofika kipindi cha pili huwa hapingwi, lakini suala hilo halipo kikatiba.

“Mimi sitarajii kugombea urais mwaka 2025, lakini kama atajitokeza mtu wa kuomba nafasi hiyo, apewe, maana ni haki yake. Kila mwanachama anayo haki ya kuchagua na kuchaguliwa,” alisema Balozi huyo.

Hata hivyo, alisema yeye hayupo tayari kuona wapinzani wakichukua nchi, kwa vile sera zao na misingi ya mapinduzi na muungano zinatofautiana, na badala yake viongozi waendelee kusimamia na kulinda misingi ya mapinduzi na muungano wa Tanganyika na Zanzibar.


Hali ya siasa na uchumi

Akigusia hali ya kisiasa na mwelekeo wa kiuchumi Zanzibar, Balozi Karume alisema sekta binafsi hasa wafanyabiashara wana umuhimu mkubwa katika kuharakisha maendeleo ya Zanzibar na hawapaswi kusumbuliwa au kuwekewa mazingira magumu ya kufanikisha biashara zao.

“Sekta ya biashara ni roho ya uchumi wa Zanzibar, wafanyabiashara wanapaswa kuwekewa mazingira rafiki ya biashara zao, tuache kuwasumbua ili kufikia malengo ya Zanzibar kuwa kituo cha biashara Afrika mashariki,” alisema.


Balozi Karume pia alizungumzia miradi ya ujenzi, akisema, inapaswa kufanyika kwa uwazi hasa utangazaji wa zabuni, ili wananchi wapate nafasi ya kufahamu mchakato wake, badala ya kampuni kutoka nje ya Zanzibar kupewa kazi kimyakimya.

Alisema kampuni za ndani za ujenzi zinapaswa kupewa kipaumbele badala ya kampuni za nje, kwa vile pesa wanazopata zitabakia nchini na kuongeza mzunguko wa fedha badala ya kuchukua kampuni ya kigeni, kwani fedha ikipatikana, husafirishwa katika nchi inakotoka kampuni hiyo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments