Lissu: Tunahitaji katiba itakayolinda haki za watu

 Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu amesema, hakuna sababu ya kuwa na mfumo mbovu wa katiba unaoneemesha wezi, inahitajika katiba mpya itakayosimamia hayo, endapo itachezewa muhusika aweze kuwajibishwa.

Lissu ameyasema hayo leo Jumatatu Mei 8, 2023 wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Kibaigwa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.

Amesema Tanzania inahitaji katiba mpya, ambayo itazuia watu kubambikiwa kesi lakini watu kutonyang’anywa mali zao na kulinda haki za binadamu.


“Nchi hii toka 2015 watu wamefungwa bure, na kunyang’anywa fedha kwa kesi za uongo na kwenda kuwekwa nje ya nchi kwa mujibu wa Rais Samia, na hakuna hata mmoja aliyekamatwa,”amesema Lissu.

Lissu ambaye alikuwa Mgombea Urais kupitia Chadema 2020, amesema kuna maneno ya uongo yanasambaa kuhusu maridhiano kwa watu ambao hawajaomba msamaha.

 “Huu upatanisho tunaoambiwa hawajabadilisha sheria hata moja, badala yake ni mabango nchi nzima kwaajili ya uchaguzi mkuu wa 2025, miaka mitatu kabla,”amesema.

 “Mbowe alikuwa gaidi juzi, leo wanapiga picha pamoja ameomba msamaha? Hawajasema kwanini walimuita gaidi, hajaeleza waliotaka kuniua, hawajaeleza walioteka watu na kuwapoteza,”amehoji Lissu.

Aidha Lissu amesema hata kwenye dini mtu hawezi kusamehewa bila kufanya kitubio, hivyo mapatano hayo na maridhiano ni kudanganya watu ili wasahau udhalimu waliofanyiwa.

 “Mimi sipingi watu kupendana, napinga kudanganywa danganywa, kupakwa mafuta kwa mgongo wa chupa na kuvikwa kilemba cha ukuta, suluhisho ni katiba mpya ikitushinda tumekwisha,”amesema.

Amesema ili kupata katiba mpya ni kujifunza kupiga kelele kudai katiba mpya, na maridhano wanayohitaji ni katiba mpya na kama ni kitu kingine na kuwa na mfumo mpya wa mtu kupita bila kupingwa.


“Maridhiano mengine ni kuwa na tume huru ya uchaguzi, kuwa na wenyeviti wa mitaa na vitongoji wanaotokana na kura zetu, sio wanotokana na wengine kenguliwa lakini pia kuwa na viongozi wanaopatikana bila kupingwa, kila mtu apigiwe kura,”

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments