Majaliwa afuta ‘task force’ Kariakoo, akemea dharau TRA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hakuna mtumishi yeyote wa umma mwenye mamlaka ya kudharau maagizo yanayotolewa na viongozi wake.

Majaliwa ametoa leo Jumatatu Mei 15, 2023 alipokuwa akizungumza na wafanyabishara wa Kariakoo kufuatia mgomo walioutisha kutokana na kero mbalimbali wanazodai zinatokana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Baadhi ya kero walizotaja wafanyabiashara hao ni kamata kamata ya TRA dhidi ya wafanyabiashara na wateja kutoka nchi jirani wanaofanya manunuzi katika soko hilo na ulazima wa kusajili maghala yanayohifadhi bidhaa kitu ambacho kimekuwa kero na kukosa majibu kwa viongozi waliofika sokoni hapo.


Asubuhi Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla aliwasili Kariakoo kuwasikilza wafanyabiashara hao akiwataka kufungua maduka  huku akiiagiza TRA isitishe mambo yote yaliyolalamikiwa, Hata hivyo wafanyabiashara hao walisema hawawezi kufungua kwani punde kiongozi huyo atakapoondoka watambiwa: “hayo ni maagizo ya kisiasa leta barua.”

Kutokana na hatua hiyo, Majaliwa amesema: “Hakuna mtumishi wa Serikali anayepaswa kumdharua kiongozi wake wa juu, Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. Chochote kitakachotakwa na viongozi hao ni agizo.”

Majaliwa amesema Rais anapotoa agizo wao kama wasaidizi wake wanapaswa kulitekeleza. Amesema Rais Samia aliagiza madai kodi ya miaka mitano nyuma kwa wafanyabiashara, wasidaiwe; lakini TRA wanawaambia watoe barua kuhusu suala hilo.

“Mnadai barua kwa watu wa Kariakoo, Wanapatia wapi barua ya Rais, alafu mnasema agizo lililotolewa na Rais ni la kisiasa hiyo ni dharau, na natamani nimjue huyo mtu aliyesema hivyo nishughulike naye mara moja,” amekemea Majaliwa.

Amesema Serikali ina taarifa za uwepo wa kikosi kazi kilichoundwa kuzunguka eneo la Kariakoo akisisitiza pamoja na kazi nzuri inayofanywa na mamlaka hiyo katika kukusanya kodi, Rais Samia amekemea vikosi kazi vyenye kuwa kero kwa wananchi.

Amesema ‘Task’ force zinatumika kuwasumbua wafanyabiashara na wakati mwingine zinatumika kuomba rushwa na Rais Samia hajatengua agizo lake la kupiga marufuku utaratibu huo.

“Kamishna wa TRA makusanyo ya ndani, hiyo ‘task force’ isitishwe mara moja na kama kuna umuhimu wa hicho kitu; Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba ajue na awaandalie utaratibu mzuri wa hicho mnachotaka  kitekelezwe, kwahiyo kamishna futa hiyo task force,” ameagiza Waziri Mkuu.

Majaliwa amesema kamatakamata ya wafanyabIashara  na wateja  inachangia kuua biashara na maduka mengi yatafungwa,

“Mfanyabiashara anadaiwa kodi mpelekee notisi na unapompelekea notisi kama amedhamiria kulipa kodi atalipa. Kamishna wa mapato ya ndani imarisha kitengo chako cha elimu kamatakamata inafukuza biashara na mbaya sana mnakamata na wageni wetu kutoka nje,”amesema.

Awali akizungumza, Mwenyekiti Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Martin Mmbwana amesema kilio chao ni cha nchi nzima kwani kila mfanyabiashara anayeingia Kariakoo lazima ashughulikiwe na mamlaka hiyo.

“Kuna suala alilozungumza Rais Samia kuhusu  kodi miaka ya nyuma tulishukuru na kupiga vigelegele lakini  TRA wanakuambia alizungumza jukwani hakuna barua, wanakutandika milioni mbili au nne, kwanza wanatuma vijana wadogo wasio na uzoefu wanatufanya shamba darasa,” amesema.TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments