MBOWE, ZITTO WATOA YA MOYONI KUHUSU MEMBE, WASEMA ALIKUWA RAFIKI WA KWELI

 MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) Freeman Mbowe na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe wametoa ya moyoni kuhusu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe aliyefariki dunia jana Mei 12 katika Hospitali ya Kairuki jijini Dar es Salaam.


Wakizungumza leo wakiwa nyumbani kwa marehemu Membe, wamesema pamoja na kwamba wao ni wa vyama vya upinzani lakini Membe alikuwa rafiki yao mkubwa na walikuwa wakifanya naye mawasiliano ya mara kwa mara pamoja na kushauriana.

 Akimzungumzia Membe, Mbowe amefafanua pamoja na kwamba walikuwa vyama viwili tofauti lakinni walikuwa marafiki.”Tumehudumu katika Bunge kwa zaidi ya miaka 15, tulikuwa na mazoea ya karibu licha kuwa na tofauti ya vyama vya siasa.

“Katika historia ya vyama vingi katika Taifa hili Membe alikuwa miongoni mwa viongozi waandamizi katika nchi yetu ngazi ya Uwaziri, hawakuwa na tabia ya kulaumu na hakuwa kada kupitiliza na kuona haki ya upande mwingine ikipokwa.

“Alikuwa rafiki yangu kwasababu tofauti za kiitikadi hazikuondoa ukweli kuwa mambo mengi tulikuwa tunashirikiana mimi na Membe.Kwa hiyo kifo chake nimekipokea kwa uchungu na masikitiko makubwa , nimepoteza rafiki, nimepoteza mwanasiasa mbobezi , nimepoteza mwanasiasa mzoefu wa kitaifa na kimataifa.”amesema Mbowe

Hata hivyo amesema binadamu wamefundishwa kutohoji mapenzi ya Mungu , ni maamuzi ya Mwenyezi Mungu na Membe imekuwa ni zamu yake, hivyo tumuombee apate pumziko la milele

“Tunaipa pole familia yake katika kipindi hiki kigumu ya kuondokewa na mpendwa wao lakini tuendelee kujitafakari huenda ikawa tunamshangaa Membe imekuwa ghafla lakini huwezi jua huenda mmoja wetu hapa akawa anafuata , hivyo tuendelee kujiwekea hazina ya uhakika za siku za usoni,”amesema.

Aidha amesema Mbowe amesema Membe ameacha somo kuwa ipo haja ya kutofautisha taasisi wanazofanyia kazi na mtu binafsi.“Sasa  siwezi kumhukumu Membe kwa kila linalofanywa na taasisi yake au Serikali , CCM imenikwaza kwa muda mrefu lakini haiondoi ukweli bado huko CCM tuna marafiki.”

Kuhusu nje ya siasa, Mbowe amesema Membe alikuwa ni mtu mcheshi na ilikuwa ni ngumu kumkuta amekasirika na uso wake muda wote ulikuwa na tabasamu.”Alikuwa anajitambua , hakuwa mtu mjinga mjinga, ana uzoefu wa kutosha na  alikuwa anaweza kuongea na mtu yoyote.

“Hakuwahi kutukimbia, maana kuna wakati mtu wa CCM alikuwa akimuona mtu wa upinzani anamkimbia lakini Membe hakuwahi kutukimbia.

Kwa upande wake Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe amesema alikutana na Membe bungeni ambapo yeye(Zitto) alikuwa mbunge wa kawaida na Membe akiwa Naibu Waziri na mpaka baadae alikupokuwa Waziri wa Mambo ya Nje

“Kwa hiyo tumefanya naye kazi bungeni kwa takribani miaka 10 yote kabla ya yeye hajatoka bungeni   na baada ya uchaguzi wa mwaka  2015 kutokana na mazingira ya kisiasa tuliyokuwa nayo Membe alikuwa miongoni mwa wanasiasa waandamizi waliokuwa  wanapinga na hali ya siasa iliyokuwepo.

“Kwa hiyo tulikuwa na ukaribu mkubwa sana, tulikuwa na mawasiliano ya mara kwa mara tulikuwa tunabadilishana mawazo na kuna nyakati mataifa yaliyokuwa wanachaama wa Jumuiya ya Madola walimtaka aende kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola , na moja ya kazi niliyoifanya ilikuwa ni nguzungumza na moja mataifa hayo kuhusu  jambo hilo kwani mazingira ya kisiasa nchini yalikuwa hayamfanyi yeye kuwasiliana nao moja kwa moja.

“Tulikuwa na ukaribu wa zaidi ya harakati za kusimamia misingi ya demokrasia na haki za binadamu lakini vile vile kwenye masuala kama hayo ya kimataifa na baada ya kuwa amefukuzwa uanachama wa CCM tulikuwa tunawasiliana sana mpaka alipoamua kuingia ACT Wazalendo,”amesema Zitto.

Ameongeza na haikuwa bahati mbaya kujiunga kwake kwani kulikuwa na majadiliano ya muda mrefu mpaka, walivyokubaliana na akaingia kwenye chama hicho.”Baada ya uchaguzi alipoamua kutoka tuliwasiliana.Moja ya jambo ambalo tunajifunza kutoka kwa ndugu Membe ni ile hali ya kujali taasisi…

“Kwasababu mmezoea watanzania watu wengi wakiingia kwenye vyama wanatumia muda mrefu kuvisema vyama walivyokwepo kabla, na wakitoka wanatumia muda mrefu kuvisagia kunguni vyama walivyokuwepo kabla .

“Jambo ambalo ni la tofauti kwa Membe alitoka CCM kwa barua na alipoamua kuondoka kutoka ACT- Wazalendo hakubwabwaja kwenye vyombo vya habari bali aliandika barua.Hata alipoulizwa kwanini ametoka ACT-Wazalendo akasema hawezi kusema chochote.

“Kwa hiyo hata baada ya kutoka kwenye chama chetu tuliendelea kuwa na mawasiliano na hata aliporudi CCM bado tuliendelea kushauriana.Kwa hiyo nchi imepoteza sio tu mwanadiplomasia mzoefu, mbobezi, mwanasiasa mahiri lakini tumepoteza mwanasiasa mzoefu ambaye viongozi wengi wa rika letu tunaweza kujifunza kwake.

“Na hata baada ya kuwa ametangulia mbele ya haki bado kuna mambo mengi ya kujifunza. Muhimu ni kuchukua yale mema aliyoyafanya na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahala pema peponi Amina.”


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments