Mbunge Dk Chaya alilia chuo cha afya ngazi ya cheti

Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), Dk Pius Chaya ameomba Serikali kupeleka chuo cha uuguzi na ukunga kwa ngazi ya astashahada (Certificate) Stashahada (Diploma) kwani kuna uhitaji mkubwa.

Katika swali la nyongeza leo Mei 22, 2023, Dk Chaya amesema uhitaji wa vyuo hivyo kwa kada ya chini ni muhimu zaidi katika wilaya ya Manyoni ambayo pia inahitaji vyuo vingine ngazi ya juu.

Kwenye swali la msingi Mbunge huyo amehoji Serikali ina mkakati gani wa kuanza ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Singida.


Akijibu maswali hayo kwa pamoja, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga amesema Serikali inaendelea na mpango wa kupeleka huduma ya elimu ya juu katika mikoa isiyokuwa na chuo kikuu au Taasisi ya Elimu ya Juu ukiwemo Mkoa wa Singida.

Kipanga amesema kwa sasa Serikali kupitia mradi wa Higher Education for Economics Transformation-HEET imetenga jumla ya Dola 8 milioni kwa ajili ya upanuzi na ukarabati wa Kampasi ya Taasisi ya Uhasibu Tanzaina (TIA) katika Mkoa wa Singida.

“Maandalizi ya shughuli za ujenzi yameshaanza ambapo hadidu za rejea za kumpata mshauri elekezi na mkandarasi, michoro, mpango kabambe na Ripoti ya Tathmini ya Mazingira na Jamii (ESIA) vimeshaanza kuandaliwa,” amesema Kipanga.

Kwa mujibu wa naibu waziri, katika jitihada hizo za kusogeza elimu ya Juu kwenda mikoa ambayo haina taasisi hizo, Chuo Kikuu cha Mzumbe pia kupitia mradi wa HEET kimepangiwa kujenga kampasi mpya katika Mkoa wa Tanga, Wilaya ya Mkinga.

Kuhusu ujenzi wa chuo cha afya kwa ngazi ya chini, amesema bado wanajipanga kufungua Chuo cha VETA ambacho kwa siku za usoni kinaweza kuwa na mchepuo huo.

Post a Comment

0 Comments