Mbunge Mattembe ahoji maadili siku ya familia

Mbunge wa Viti Maalum Aysharose Mattembe (CCM) amehoji Serikali inatoa tamko gani kuhusu siku ya kimataifa ya familia kwa ajili ya kulinda Maadili ya Watoto wa Kitanzania ambayo katika siku za hivi karibuni yameanza kulegalega.

Mattembe amehoji jambo hilo leo Mei 11, 2023 alipouliza swali la papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu akisema ni wakati sasa wa Serikali kutoa kauli juu ya mambo hayo yasiyofaa kwenye maadili ya Mtanzania.

Mbunge amesema katika siku za hivi karibuni kumeshuhudiwa kuwepo kwa mmomonyoko mkubwa wa maadili hivyo akataka kujua nini msimamo wa Serikali katika kukomesha mambo ya mmomonyoko wa maadili.


"Mheshimiwa Waziri Mkuu, tarehe 15 Mei ni siku ya familia dunia, tumeshuhudia katika siku za hivi karibuni mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa watoto katika Jamii yetu, je Serikali inatoa kauli gani kuhusu siku hiyo," amehoji Mattembe.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Tanzania inaungana na dunia katika kuadhimisha siku hiyo kwa kuitaka jamii kusimama katika maadili mema hasa kwa watoto.

Majaliwa amesema Mei 15 ni siku chache zijazo lakini wataendelea kuhimiza maadili kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwa kushirikiana na taasisi na viongozi wengine, huku Serikali ikipinga vitendo vyote vya uvunjifu wa kimaadili. 

Waziri Mkuu amesema Serikali iko macho wakati wote katika kulinda maadili ya Mtanzania na ikiwemo kuitumia siku hiyo kukumbushana kuhusu kuzuia mmomonyoko wa maadili.

Post a Comment

0 Comments