Serikali yaendelea kufunga mlango uraia pacha

Serikali imeendelea msimamo wake wa kutokuwa na uraia pacha kwa wananchi wake waishio ughaibuni na badala yake imesema watapewa hadhi maalumu.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusufu Masauni ameliambia bunge leo Mei 15,2023 kuwa sheria hairuhusu uraia pacha kwa watu wazima isipokuwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka kumi na nane ambao wanakuwa na uraia wa Tanzania na uraia wa nchi nyingine.

Masauni alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Agnesta Lambati (CCM) ambaye amehoji kama Serikali ipo tayari kuruhusu uraia pacha kwa Watanzania wenye uraia wa nchi nyingine.


Katika swali la msingi mbunge huyo ameuliza ni kwa nini Serikali inakuwa na kigugumizi na kama itakubali ipeleke bungeni sheria hiyo ili ifanyiwe marekebisho.

Masauni amesema uraia wa Tanzania unaongozwa na Sheria ya Uraia ya Tanzania Sura ya 357 rejeo la mwaka 2002, inabainisha aina tatu za uraia wa Tanzania ambazo ni uraia wa kuzaliwa, uraia wa kurithi na uraia wa kuomba.

Hata hivyo Waziri amesema Serikali haijajiridhisha kama ni takwa la watu wengi kuomba uraia pacha ndiyo maana hata kwenye mchakato wa Katiba iliyokwama ilieleza kuwa kundi hilo litapewa hadhi maalumu.

Kuhusu watu kubaguliwa alisema siyo kweli kwani serikali inawapenda watu wake na kuwatendea haki isipokuwa sheria muhimu sikasimamiwa.

Post a Comment

0 Comments