Spika Tulia aonya wabunge wanaovua nguo bungeni

Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson amesema kitendo cha Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM) Mwita Waitara kuvua koti na tai akiwa ndani ya Bunge,” Hairuhusiwi kufanya hivyo ndani ya Bunge na huo ni utovu wa nidhamu.”

Dk Tulia ametoa kauli hiyo usiku wa leo Jumanne, Mei 9, 2023 wakati akihitimisha kikao cha Bunge jijini Dodoma akirejea kilichojitokeza asubuhi wakati wa kipindi cha maswali na majibu.

Mbali na kuvua koti na tai bungeni, Waitara alilia kwa kile alichokisema amepewa majibu ya uongo kuhusu fidia ya wakazi wa Tarime, Mkoa wa Mara, waliokuwa wakitakiwa kupisha mgodi wa Barrick North Mara.


Waitara aliyewahi kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na naibu Waziri ofisi ya Muungano na Mazingira alionyesha hasira zake kwa kuvua koti alilovaa na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.

Akijibu swali hilo, Byabato alisema mgodi huo ulionesha nia ya kutaka kuchukua baadhi ya maeneo ya vijiji hivyo ambavyo ni sehemu ya vijiji vinavyozunguka mgodi huo.

Hata hivyo, alisema baada ya wakazi hao kupata taarifa ya maeneo yao kuhitajiwa na mgodi wa Barrick North Mara, walianza kuongeza majengo haraka haraka (maarufu kama Tegesha).

Baada ya majibu hayo, Waitara alipewa nafasi ya kuuliza maswali la nyongeza ambapo alieleza kusikitika kutokana na majibu ya Serikali kwa kusema, “Naomba nisikitike sana kumbe watu wa Tarime wajue adui wao mkubwa ni nani?”

Kutokana na tukio hilo, Dk Tulia alisema Waitara kama hakuwa ameridhika na majibu ya majibu kanuni ziko wazi na kueleza alipaswa kufanya nini, lakini hakufanya hivyo na kuamua kutoka ukumbini akiwa amevua koti na tai.

“Hairuhusiwi kufanya hivyo ndani ya Bunge na huo ni utovu wa nidhamu. Kanuni zetu zinaelekeza jinsi ya kuvaa humu bungeni,” alisema Dk Tulia na kuongeza:


“Huko nyuma imewahi kujitokeza mtu anapiga magoti, anapiga sarakasi, sasa hii ya kutoa nguo, hapa hairuhusiwi na isijirudie tena, kama una hasira kazitolee nje.”

Kilichofanywa na Waitara kulia ndani ya Bunge kumewahi shuhudiwa pia kwa wabunge Faida Bakari (Viti Maalum-CCM) na aliyekuwa Mbunge wa Tandahimba kupitia CUF, Ahmad Katani ambaye sasa yupo CCM.

Hilo lilitokea baada ya Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato kujibu swali la msingi la Waitara kwa niaba ya Waziri wa Madini, Dk Doto Biteko.

Katika swali lake la msingi, Waitara alihoji ni lini wananchi wanaodai fidia katika maeneo ya vijiji hivyo watalipwa.

Waitara alisema Dk Biteko wakati akihitimisha hoja yake ya bajeti ya mwaka 2023/24, Machi 28, 2023, alisema haitafikia Juni, 2023 watakuwa wameshalipwa.

Pia alisema mgodi huo umemwambia wameenda kuomba katika bodi fedha ili watu walipwe lakini Serikali katika majibu yake bungeni jana ilisema maeneo hayo yaliyokaa miaka 11 bila kuendelezwa hayahitajiki kwa kuwa mgodi hauathiriki.

“Wananchi wangu waendelee kuathirika kiuchumi na kisiasa, haya majibu ni ya maumivu makubwa kwa watu wa Tarime. Nataka nitangaze wananchi wa Tarime wawajue mbaya wao ni nani pamoja na yote yanayoendelea pale Tarime,”alisema.

Kauli hizo zilimfanya Mwenyekiti wa Bunge, David Kihenzile alimwambia kama hakuwa na swali basi akae chini lakini yeye alisema hakukuwa na majibu hapo na kuwa majibu yaliyotolewa ni ya uongo kabisa.

Huku akiendelea kulalamika, Katibu wa Bunge alizima kipaza sauti chake lakini Waitara aliendelea kulalamikia majibu ya Serikali wakati akianza kulia.


Hali hiyo iliwafanya wabunge wenzake waliokuwa wameketi karibu naye, kumtuliza huku wakimpa pole, hatua ambayo ilisababisha shughuli za Bunge kusimama kwa muda.

Wakati akiendelea kulalamika mambo mbalimbali yanayoendelea kwenye jimbo lake bila kipaza sauti, Kihenzile alimtata Waitara kufuata utaratibu kama swali lake halijajibiwa vizuri na Serikali.

Kanuni za Uendeshaji wa Bunge, zinamtaka mbunge ambaye hakuridhika na majibu ya waziri kuomba mwongozo wa Spika kueleza kutoridhika kwake.

Kifungu cha 53(4) cha kanuni hizo kinasema, iwapo Spika ataridhika kuwa, swali la msingi au la nyongeza halijapata majibu ya kuridhisha, ataagiza lijibiwe kwa ufasaha zaidi katika kikao kingine cha Bunge.

Hata baada ya Kihenzile kumtaka kufuata utaratibu, Waitara aliendelea kulalamika kuhusu mambo mbalimbali yanayoendelea Tarime huku Bunge likiwa limetulia kwa sekunde kadhaa.

Baada ya sekunde kadhaa, Waitara alionekana akifungasha vitu vyake na baadae alianza kuvua koti kisha kubeba vitu vyake na kuanza kuondoka, huku akiwa ameshikilia koti lake mkononi.

Baada ya hapo, kipindi cha maswali na majibu kiliendelea ambapo Kihenzile alimuita Mbunge wa Liwale (CCM), Zuberi Kuchauka kuuliza swali lake la msingi ambapo alitaka kufahamu ni lini itafungua ofisi ya madini Wilayani Liwale.

Swali hilo liliendelea kujibiwa na Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato kwa niaba ya Waziri wa Madini Dk Doto Biteko ambapo alisema miongoni mwa vigezo vya kufungua ofisi ya madini ni uwepo wa shughuli kubwa za madini katika eneo husika.


Byabato alisema kwa sasa shughuli za madini katika Wilaya ya Liwale ziko chini kuliko wilaya za Ruangwa, Kilwa na Nachingwea na hivyo wakazi wa Liwale wanashauriwa kutumia ofisi za madini zilizopo Lindi Mjini na Nachingwea.

Hata hivyo, baada ya majibu hayo kulikuwa na minongono inaendelea bungeni, hali iliyomfanya Kihenzile kuwataka mara kadhaa wabunge kutulia kabla ya kuruhusu swali la nyongeza.

“Waheshimiwa wabunge naomba tutulie, waheshimiwa wabunge wote naomba tutulie.Na kiti kikisimama wote mliosimama ama kutembea mnatakiwa mkae kabla sijawataja kwa majina,”alisema kabla ya kuruhusu swali la nyongeza kwa Kuchauka.

Akiuliza swali, Kuchauka alieleza kusikitishwa na majibu ya waziri ambayo hajamridhisha yeye wala wananchi wa Liwale.

Lakini sakata hilo, liliendelea baada ya Mbunge wa Rorya (CCM) Jaffar Chege kuomba mwongozo wa Spika wa Waitara kutoridhishwa na majibu ya Serikali na yale yaliyotokea bungeni ambayo yalizua taharuki ndani ya Bunge.

Akijibu mwongozo huo, Kihenzile alisema watapitia hoja ya Waitara na Chege ili kuona kama kilichotokea kinaruhusiwa ama hakiruhusiwi na Bunge na baadaye watalitolea mwongozo.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments