TAASISI YA SISI TANZANIA MKOA WA SINGIDA YAWAKUTANISHA VIONGOZI KATIKA KIKAO KAZI

Taasisi ya isiyoya Kiserikali ya Sisi Tanzania Mkoa wa Singida imewakutanisha viongozi wote wa taasisi hiyo kutoka wilaya zote saba za Mkoa wa Singida, katika kikao kazi chenye lengo la kujadili masuala yao pamoja na kampeni kadhaa walizozipanga kuzifanya.


Akizungumza kwenye kikao hicho kilichofanyika May 13, 2023 Mratibu wa taasisi hiyo Mkoa wa Singida, Shabani Mukee alisema baadhi ya kampeni hizo ni kuwatembelea wahitaji waliopo kwenye makundi maalum kama wajane, wagane na yatima kwa ajili ya kufanya hisani kwa kutoa misaada ya kijamii.

Alisema walengwa wengine wa kampeni hiyo ni wanafunzi ambao wapo pembezoni ambao kwa namna moja ama nyingine wanashindwa kwenda shuleni kutokana na changamoto mbalimbali.

"Sisi Tanzania Mkoa wa Singida tumejipanga kuwafikia watoto wenye changamoto hizo wakiwemo waliopo katika mazingira magumu na kuhakikisha mahitaji yao yanatimizwa kadri Mwenyezi Mungu atakavyotusaidia," alisema Mukee.

Mukee alisema ajenda nyingine walioijadili ni suala zima la kuwaandaa vijana kuja kuwa viongozi hivyo wanatarajia kuendesha semina kwa vijana wa Mkoa wa Singida na anaamini baada ya mwaka mmoja watapatikana vijana wengi ambao watakuwa viongozi katika kada mbalimbali na baadhi yao kujitokeza katika chaguzi za mbeleni kugombea nafasi za uongozi.

Alitaja mkakati mwingine kuwa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kupanda mti kwenye kila kwaya ambao utaitwa mti wa mkuu wa kaya ambao utapandwa katika kila nyumba iliyopo Mkoa wa Singida ili kuufanya mkoa mzima kuwa ni wa kijani.

Alisema taasisi hiyo inaamini kampeni hiyo ikifanikiwa itaisaidia serikali katika kukabiliana na tabia nchi kwa kuhifadhi mazingira.

Alisema viongozi walioudhuria kikao hicho walitoka wilaya ya Mkalama, Iramba, Manyoni, Itigi, Ikungi, Singida DC na Manispaa ya Singida.

Katibu Mkuu Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Singida, Emmanuel Digha alisema vijana wana umuhimu wa kujiunga na taasisi hiyo inawaunganisha kwa pamoja kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazowahusu na kuzitafutia ufumbuzi.

"Umuhimu wa vijana kujiunga na Sisi Tanzania itatusaidia vijana kupeana fursa mbalimbali na kuelezana changamoto zinazo tukumba na hatimaye tuweze kulijenda taifa katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa," alisema Digha.

Naye Hellen Pascal ambaye ni Mratibu wa Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Singida alisema Sisi Tanzania mkoani Singida inawaunganisha vijana wote waliopo katika vyuo mbalimbali vya Serikali, watu binafsi na taasisi za dini.

Alisema wanawakutanisha vijana ili wazielewa fursa zilizopo ndani ya taasisi hiyo kutokana na vijana wengi kutozifahamu ili wazijue na kuzitumia waweze kutoka kimaisha.

Mjumbe wa taasisi hiyo Gwau Msafiri alisema kazi nzuri ya kutoa hisani kwa makundi yenye uhitaji inayofanywa na Sisi Tanzania ni ya muhimu kwa jamii ambapo alitoa ushauri kuwafikia na walengwa ambao hawafikiwi kutokana na kuishi maeneo ya pembezoni.

" Mara nyingine watu wenye mahitaji ambao ufikiwa ni wale ambao wapo kwenye miji na shauri twende mbele zaidi kwa kuwafikia waliopo pembezoni mwa miji ambako kuna watu wenye changamoto nyingi ukilinganisha na wale waliopo kwenye maeneo ya mijini," alisema Msafiri.

Mratibu wa taasisi hiyo Wilaya ya Singida Mjini Masanja Sitta alisema wao wamejikita kutembelea vyuoni na mashuleni kuhamasisha wanafunzi kuzingatia maadili na kupinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia na kutojiingiza katika ndoa za jinsia moja na usagaji.

Afisa Miradi wa taasisi hiyo Mkoa wa Singida, Abdallah Shabani alisema kutokana na changamoto kubwa ya ajira kwa vijana tumejipanga kuibua miradi ambayo itakuwa chachu na fursa kubwa kwao hasa katika miradi ya kilimo ambayo taasisi yetu inatarajia kuanzisha mashamba darasa katika kila halmashauri.

"Nina amini vijana wakipewa nafasi kubwa ya kujitegemea itakuwa mkombozi kwa wao kujiondoa kifikra na kujipambanua zaidi kimaendeleo kuanzia mtu mmoja mmoja na jamii inayowazunguka kiujumla," alisema Shabani.

Mhasibu wa Taasisi hiyo Mkoa wa Singida, Hadija Misanga, alisema pamoja na mipango yote hiyo alisema wana programu ya kutoa mafunzo kwa vijana wenye umri wa chini ili kujua nini maana ya uongozi na kuwafanya baadae wawe viongozi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments