Tanzania yamteua Dk Tulia kuwania Urais IPU

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameteuliwa na Tanzania kuwania Urais wa Umoja wa Mabunge la Dunia (IPU) katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba, 2023.

Uteuzi huo, umetangazwa leo Alhamisi, Mei 11, 2023 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax baada ya kikao na mabalozi wa nchi mbalimbali kuhusu Tanzania kuwania nafasi hiyo.

Iwapo Dk Tulia ataukwaa wadhifa huo, atakuwa mwanamke wa kwanza kuliongoza Bunge hilo, lenye nchi wanachama 179 na wabunge 705 wanaoziwakilisha nchi zao.


“Katika jitihada zetu za kumnadi mgombea, tumeona lazima tukutane na majirani zetu na ombi letu limepokelewa vizuri na wenzetu ambao wanafahamu uwezo wake,” amesema Dk Tax.

Kwa sababu inayowania nafasi hiyo ni Tanzania, Dk Tax aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), amesema ni jukumu la kila mmoja kwenye nafasi yake kumnadi Dk Tulia katika wadhifa huo anayowania.

Maboresho ya kuhakikisha changamoto za dunia zinakoma, kuimarisha amani, kuhamasisha wanawake kuwa sehemu ya maendeleo na uongozi ni miongoni mwa vipaumbele vya Dk Tulia kwa mujibu wa Dk Tax.

“Anatarajia kuboresha uhusiano ndani ya Umoja wa Mataifa (UN) kwa sababu wanachama wa IPU ni wanachama wa UN,” alisema.

Kwa mujibu wa waziri huyo, nafasi hiyo itaitangaza Tanzania kimataifa na kupata nafasi ya kuyasimamia masuala yenye maslahi ya kidunia.

Uteuzi wa Dk Tulia kuwania nafasi hiyo, umetokana na kile kilichoelezwa na Dk Tax kuwa anastahili kutokana na uwezo na uzoefu alionao kwenye uongozi.

Bunge hilo lililoanzishwa mwaka 1889 kama kundi dogo la wabunge waliopigania amani, kwa sasa Duarte Pacheco kutoka Ureno ndiye anayeliongoza kwa nafasi ya urais.
Akizungumzia hilo, mwakilishi wa Tanzania katika IPU, Elibariki Kingu amesema nafasi hiyo ni muhimu kwa nchi kwani nafasi hiyo inakuwa na wadhifa kubwa kwenye mashirika ya kimataifa.


“Tukiweka ajenda hii mbele kwa maslahi ya nchi, tutaitangaza nchi na kuinua diplomasia na kutoa nafasi ya kuonyesha Tanzania inathamini malengo ya dunia ya kumpa nafasi ya uongozi mwanamke,” amesema.

Kulingana na utaratibu wa IPU, Kingu amesema nafasi hiyo inaongozwa kwa miaka mitatu, kisha anafuata mwingine.

Kingu ambaye pia ni mbunge wa Singida Magharibi (CCM), amesema usikivu, uwezo, malengo makubwa ni miongoni mwa sifa alizonazo Dk Tulia.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments