Tido: Vyombo vya habari 'taabani,' sawa na mgonjwa ICU

Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Media Group, Tido Mhando amesema ukata katika vyombo vya habari nchini waweza kuwa sababu ya kurushwa kwa maudhui mengi ya nje ambayo wakati mwingine hubeba kisichofaa kwa jamii.

Ameyasema hayo leo katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa minara ya kurusha matangazo ya Televisheni ardhini (DTT) ya kampuni ya Azam Media Limited jijini hapa.

Akijaribu kutafuta maneno sahihi ya kuelezea hali hiyo ya uchumi mbaya, Mkurugenzi huyo Amesema: “…huenda hayatumiki maneno sahihi ya kuelezea suala hilo lakini ingekuwa afya ya binadamu basi wangeweza kusema vyombo vya habari nchini viko katika hali taabani na hali yao ni mahututi.”


Mhando amesema ukweli ni kuwa vyombo vya habari vimekuwa vikishindwa hata kugharamia matakwa ya kisheria ya leseni na kuchakata maudhui ya ndani kiasi cha kuwalisha wateja maudhiu ya nje yasiyo na maadili.

"Wengine saa hizi imebidi waende wachukue vipindi vya nje ambavyo maudhui yake hayana hadhi hapa nchini kwa sababu hawana uwezo wa kulipia gharama za kutengeneza vipindi hapa ndani," amesema Mhando.

Amesema mfumo uliowekwa na mamlaka unavitaka vituo vya matangazo ikiwemo televisheni vipate mapato yake kutoka katika matangazo ya kibiashara ili walipe waliojenga minara ya kurusha masafa.

Lakini vituo husika vimekuwa vikishindwa kulipa kwa sababu ya kukosa mapato ya kutosha ambayo wamekuwa wakiyakusanya kutoka matangazo ya biashara.

"Nadhani sasa hivi imekuwa ni habari za kawaida kusikia kulikuwa na mizozo ya wafanyakazi kwa vyombo vya habari kuzozana na wawekezaji na wenye mali kwa sababu wameshindwa kulipa mishahara, wawekezaji na wenye mali siyo kwamba hawataki kufanya hivyo lakini hali halisi ndiyo imesababisha matokeo haya,” amesema.

Hivyo basi, Mhando Amesema umefika wakati tasnia ya habari kwa ujumla iweze kutupiwa jicho ambalo linaweza kutatua changamoto hiyo kwani hawaoni sababu ya kufikia hapo.


Amesema hali hiyo imewalazimu wamiliki wa minara kutumia njia ya kubadilishana bidhaa badala (butter trade) ya malipo.

"Imebidi sasa tusaidiane, tumefika hali ya nipe nikupe," amesema Mhando. Hivyo ameitaka serikali kuridhia mapendekezo yaliyowasilishwa kwa mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) kwa ajili ya utekelezaji na kwamba ziwepo jitihada za pamoja ili kuangalia namna ya kuimarisha hali hizo.

Akiwa kama Mwenyekiti wa kamati ya kufanya tathmini ya hali ya uchumi wa vyombo vya habari iliyoundwa na Waziri wa Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Nape Nnauye hatua za mwanzo zinaonyesha kuwa bila ya serikali kuingilia kati suluhisho halitapatikana.

"Tumeshaanza kuongea na wenzetu, ili waweze kutuambia kwanini tumefika hapa, na bila ushirikiano wa pamoja na Serikali baadhi ya vyombo hivi ambavyo ni kuhimu katika maendeleo ya nchi vitazidi kuzorota," amesema Mhando.

Akizungumzia mradi uliozinduliwa leo alisema uwekezaji wake hadi sasa umegharimu Sh50 bilioni na umesheheni miujiza ya kuweza kufanikisha utangazaji na maendeleo ya baadaye yaani ‘5G broadcast’ ambapo chaneli za televisheni zitaanza kuonekana katika simu ya mkononi bila kutumia ‘App.’

Uzinduzi huo umeenda sambamba na maadhimisho ya miaka 10 ya Azam Media na kwamba uwekezaji huo unaashiria manufaa ya baadaye nchini kwa kipindi cha sasa na kijacho.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments