Waziri Mkuu Majaliwa kushiriki kongamano Wiki ya Madini

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kesho Mei 9, 2023, atashiriki kongamano maalum la kujadili maendeleo ya sekta ya madini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Madini yanayofanyika Kitaifa jijini Mwanza. 

Kupitia kongamano hilo litakaloshirikisha wachimbaji wadogo, wafanyabiashara na wanunuzi wa madini, wawakilishi kutoka vyama vya kisekta na watoa huduma mbalimbali katika sekta ya madini nchini Tanzania watawasilisha kwa Waziri Mkuu hoja, changamoto na ushauri wa namna ya Serikali kushirikiana na wadau wengine kuyapatia ufumbuzi.

Maadhimisho ya Wiki ya Madini yanayoambatana na maonyesho ya zana, vifaa na shughuli mbalimbali zinazohusiana na sekta ya madini yanafanyika jijini Mwanza tangu Mei 4, 2023.


Zaidi ya washiriki 1, 500 ambao ni wanachama wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo Tanzania (Femata) watashiriki kongamano hilo.

Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa amewaambia waandishi wa habari jijini Mwanza leo Mei 8, 2023, kuwa kongamano hilo ni fursa muhimu kwa wadau wa sekta ya madini kuwasilisha hoja, changamoto na maoni yao kwa Serikali kwa ajili ya utekelezaji.

Amesema ni matarajio ya Serikali kuona kongamano hilo likitumika siyo tu kutangaza sekta ya madini, bali pia kuifungamanisha na sekta na huduma za kiuchumi kwa maendeleo na ustawi wa Taifa.

"Kupitia kongamano hili, fursa nyingi zinatambulishwa na wadau, na Serikali iko hapa siyo tu kuwatia moyo wachimbaji wadogo, bali pia kushirikiana nao kutatua hangamoto kutokana na umuhimu na mchango wa sekta ya madini katika maendeleo ya Taifa,’’ amesema Naibu Waziri Kiruswa

Rais wa Femata, John Bina amesema kupitia majukwaa tofauti ikiwemo maadhimisho ya Wiki ya Madini, wachimbaji wadogo, watoa huduma, wafanyabiashara na wanunuzi wa madini tayari wamewasilisha hoja na maoni zaidi ya 100 ambayo baadhi yameshafanyiwa kazi na Serikali.

"Femata tunaamini katika mashauriano na majadiliano yenye nia njema na kuaminiana katika kutafuta na kupatia ufumbuzi changamoto zinazoikabili sekta ya madini tunafurahia uwepo wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika kongamano letu la Mei 9, 2023. Tunaamini Serikali itapokea hoja na maoni yetu na kuzifanyia kazi,’’ amesema Bina

Akizungumzia maadhimisho, maonyesho na kongamano la wadau wa madini mwaka huu, Henry Joseph, mchimbaji na Meneja wa kampuni ya Godmwanga Gems amesema ushiriki wake umemwezesha kubaini fursa nyingi za uwekezaji na biashara zinazopatikana kwenye uchimbaji wa madini ya Graphite ambayo ni miongoni mwa madini ya kimkakati.

"Madini haya ni ya kimkakati kwa sababu yanahitajika kote duniani kwa ajili ya kutengeneza betri za magari yanayotumia umeme; hii ni fursa nzuri kwetu kwa sababu Tanzania ni miongoni mwa Mataifa yenye utajiri wa Graphite ikishika nafasi ya sita duniani kwa kuwa na kiwango kikubwa cha madini haya,’’ amesema Henry ambaye kampuni yake inachimba madini hayo


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments