Abubakar Bakhresa afunguka miaka 10 ya milima, mabonde Azam

Mkurugenzi Mtendaji wa AML, Abubakar Salim Bakhresa anasema ilianza kama mzaha, wakiwa wanaangalia moja ya mechi za timu ya Azam.

"Tulipata wazo pale, baada ya kujiuliza tutawezaje kuiangalia timu yetu ikicheza hata kama iko mbali? Tukawauliza wadau wa masuala ya utangazaji ni njia zipi tunaweza kuzitumia kuangalia mechi za timu yetu mubashara?


"Haikuwa rahisi, ingawa baadaye tulikutana na watu wa Star TV ambao walikuwa na ‘OB Van’ (gari la kurusha matangazo ya nje), tukawaomba kwa kutumia gari lao ili mechi za Azam FC zirushwe mubashara.

"Walikubali, lakini ilikuwa ni lazima TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) ishirikishwe, tulifanya hivyo wakakubali na baadhi ya mechi zetu zikaanza kuonyeshwa, lakini kwa kulipia, tena kwa gharama kubwa," anasema.

Anasema walifurahia hatua hiyo, lakini shauku yao haikufanikiwa kwa kuwa OB Van ilikuwa ndogo. Wakati hayo yakifanyika, Bakhresa anasema ziliibuliwa tuhuma zikihusisha ushindi wa Azam na ununuzi wa mechi.

Anasema tuhuma za ununuzi wa mechi ziliwafikirisha zaidi na kuona kuna fursa ya biashara kwa kutangaza mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Tuliona kwa kufanya hivyo uhalisia utaonekana na kuonyesha ipi ni timu bora, hata hivyo changamoto ikawa kwa wawekezaji kutoonyesha nia, japo wakati huo kulikuwa na kampuni iliyorusha mechi za Simba na Yanga kwa kutumia OB Van kutoka nje.

"Tulihoji kwa nini wasifanye hivyo kwa ligi yote? Lakini jibu jepesi likawa kwamba hawana ‘interest’. Tulishangaa, lakini kipindi hicho tukiendelea kufanya kazi na Star TV ndipo dunia ilikuwa ikihama kutoka kwenye analojia kwenda dijitali,” anasema.


Bakhresa anasema waliamua kuanzisha AML, hata hivyo hofu ilikuwapo kwa kuwa tayari kulikuwa na waliowatangulia na walishajiimarisha.

"Tulipata mtaalamu mshauri kutoka Uingereza tukampa kazi, kipindi hicho dunia ilijielekeza kwenye mfumo wa kurusha matangazo kwa kutumia minara (DTT) na ile ya satelaiti, yaani DTH.

"Ushauri wa mtaalamu wetu ulikuwa tuanze na mfumo wa DTT (minara na antena), ingawa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wakatushauri tofauti kwamba tunaweza kuomba leseni ya DTH kama wawekezaji wa nje kwa sababu leseni za DTT zilikuwa tatu pekee na tayari zilishachukuliwa na wawekezaji wengine,” anasema.

Miaka 10

Anasema katika harakati hizo hadi sasa wanatimiza miaka 10, walipitia vipindi vigumu kwa nyakati tofauti, ikizingatiwa wao ndio walikuwa wa kwanza kuanzisha televisheni ya malipo Tanzania.

Anasema uratibu wake ulikuwa mgumu kwa upande wa TCRA kwa sababu uzoefu ulikuwa katika kuratibu chaneli za kawaida za bila malipo. "Ilichukua muda kwa TCRA kufanya mabadiliko, maana wakati fulani ilikuwa ni ngumu hata kututafsiri tuko kundi gani, kati ya televisheni ya malipo au bure.

"Kuna kipindi kilifika tukaondoshewa chaneli zote za ndani kwenye kisimbuzi chetu, wakati wao ndio wadau wetu muhimu. Hali hii ilitutia hofu sana kiasi cha kujiuliza kwa nini tumeingia kwenye biashara hii?” anasema.

Bakhresa anaongeza: "Hata hivyo, tunaishukuru Serikali baada ya mjadala, kukafanyika mabadiliko katika mfumo wa biashara ya televisheni Tanzania na ikaona kuna umuhimu wa kuwa na mwekezaji wa nne kwenye mfumo wa DTT. Ilipotangazwa zabuni na sisi tukaomba na tukafanikiwa kupata leseni inayotufanya sasa kuwa wakubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

"Tunamshukuru Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuja kutuzindulia mfumo wetu wa matangazo ya kutumia minara (DTT), kama nilivyosema tulianza kwa kurusha matangazo kwa mtindo wa satelaiti (DTH), sasa tunatumia DTT, huduma iliyotugharimu dola za Marekani milioni 20 (zaidi ya Sh47 bilioni), alisema Bakhresa wakati wa uzinduzi uliofanyika Mei 18, mwaka huu.

"Wakati ule ungeniuliza kuhusu DTT jibu langu lingekuwa siyo lazima, lakini sasa nasisitiza ni ya muhimu kwa nchi kwa sababu, kwanza kuna uhakika wa usalama.

"Mfano leo kwa sababu zozote ikitokea satelaiti haifanyi kazi, maana yake ni kwamba hakuna mawasiliano ya matangazo, lakini watu wenye DTT wataendelea kutoa huduma. Kwa hiyo, kwa usalama wa nchi kwenye sekta ya utangazaji DTT ni muhimu na inatupa uhakika na kutokuwa tegemezi kwa miundombinu ya nje.

"Kitu kingine ambacho ni cha muhimu zaidi ni kwamba, baada ya teknolojia ya matangazo kwa mfumo wa 5G kuimarika duniani, kupitia DTT watu wataweza kufuatilia matangazo kwa kutumia simu zao za mkononi bila kutegemea kifurushi cha intaneti.

Matangazo ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania

Anasema mwanzo wa biashara hiyo ni mpira na walipoomba haki ya kurusha matangazo, TFF ilikubali na ukawa mwanzo wa maudhui ya ndani.

“Mpira ukaonekana na kuwa biashara na kuendelea kutazama fursa nyingine kwenye tamthilia na filamu za ndani, na taarifa za habari.

“Sisi kama wawekezaji tukaona kuna haja ya kutafuta mtazamo wa pamoja wa kuitambua thamani ya ligi yetu, wakati ule wa michakato ya kununua haki za matangazo ya mpira, hatukueleweka mara moja hasa na timu kubwa za Simba na Yanga, kwa sababu hawakuridhika na aina ya mkataba tulioingia na TFF, lakini sisi tukasema ligi hii ina thamani, lakini ukubwa wa thamani yake hauwezi kuonekana sasa kwa sababu unajengwa,’ anasema mkurugenzi huyo, huku akiitabiria kampuni hiyo kuwa miongoni mwa kampuni kubwa za habari Afrika.


"Tuliona sisi tunawekeza, watakuja wengine watawekeza, ni wazi thamani ya ligi itapanda na kila mmoja atanufaika. Hiki ndicho kinachotokea kiasi cha kupata imani ya Simba na Yanga ambao wanakiri kwamba mkakati uliotumika ulikuwa sahihi kutufikisha hapa tulipo,” anasema.

Bakheresa anasema, "Katika harakati hizo, siku moja nilikaa na wenzangu nikasema mpira wa Uingereza umeendelea kwa sababu unaonekana na kujadiliwa kila siku. Nikasema Tanzania lazima twende huko na sasa ni sehemu ya utamaduni wetu.Naweza kuandika kitabu kikubwa ninapoizungumzia safari ya mapinduzi ya soka Tanzania na namna tulivyofanikiwa kuiongeza thamani ya ligi yetu.

Miaka 10 ijayo, Bakhresa anasema anaiona Azam Media kuwa miongoni mwa kampuni kubwa za matangazo barani Afrika itakayofanya mapinduzi makubwa ya mpira wa Tanzania kufikia kuwa na ligi bora Afrika.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments