ACT yajitosa bajeti Wizara ya Nishati, ikiionyooshea kidole Serikali

Siku moja baada ya Wizara ya Nishati kuwasilisha Bungeni bajeti yake Chama cha ACT Wazalendo kimeibuka na kusema ngumu kukamilisha miradi ya maendeleo ikiwa Wizara inapata kiasi kidogo cha fedha hali ambayo inafanya miradi mingi kususasua.Akifafanua hayo Msemaji wa Sekta ya Nishati wa chama hicho Isihaka Mchinjita kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa leo Juni 1, 2023; Chama hicho amesema hoja hiyo inathibitika kwa chambuzi mbalimbali za bajeti zilizopita za wizara hiyo.

“Kwa mwaka wa fedha 2020/2021 Wizara ilipanga kutumia Sh2.1 trilioni lakini hadi kufikia Aprili 2021 ilipokea Sh1.3 trilioni sawa na asilimia 61 ya bajeti yote na kwa mwaka 2021/22 Wizara ilipanga kutumia Sh2.3 trilioni hata hivyo ilipewa Sh1.8 trilioni sawa na asilimia 76 ya bajeti yote katika kipindi kama hicho.

“Pia kwa mwaka 2022/23 ilionyesha namna Serikali inavyotawanya nguvu kiduchu ya fedha iliyopo katika kutekeleza miradi mingi ya kuzalisha na kusafirisha umeme ambayo mingine kwa zaidi ya miaka saba sasa imekuwa ikitajwa kama miradi ya kipaumbele bila kutengewa fedha za utekelezaji wake au mingine kutengewa fedha kidogo,” amesema 

 kutokana na utitiri wa miradi Serikali imeweza kukamilisha mradi mmoja tu wa Kinyerezi (MW185) ambao umechukua miaka nane tangu 2015.Mchinjita anaendelea kusema katika mwaka wa fedha 2023/24 wameona Serikali ikiendelea na utaratibu ule ule wa kuorodhesha utitiri wa miradi na kutawanya fedha bila kukamilisha malengo.

Amesema orodha ya baadhi ya miradi ya kipaumbele iliyopo kwenye hatua ya utekelezaji na kutengewa fedha kwa mwaka huu ni mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Julius Nyerere (JNHPP) MW 2,115 uliotengewa Sh1.5 trilioni, mradi wa Kuzalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia Mawe Project (MW 150) zimetengwa Sh345 bilioni.

Amesema pamoja na mingine mingi kwa ujumla wake inagharimu Sh17 trilioni ambapo malengo ya Wizara wakati inaianzisha miradi hii ilikuwa ikamilike ifikapo mwaka 2025.

“Kwa mwenendo huu wa bajeti ambapo mpaka sasa wizara haijapata hata asilimia 30 ya fedha inazozihitaji kukamilisha miradi hii, ndoto ya kuzalisha MW 5000 za umeme ifikapo 2025 haziwezi kufikiwa huku baadhi ya miradi ikikumbwa na harufu za rushwa na uzembe unaoligharimu taifa,” amesema.

Mwisho ACT wameitaka Serikali ijikite kwenye miradi michache itakayotoa matokeo kwa kuzingatia uwekezaji ambao umeshafanyika vilevile ijikite kwenye uwezekano wa nchi kujitosheleza kwa nishati ya umeme kabla ya kufikiria kuuza umeme nje ya nchi.“

Kwa kufanya hivi tutaokoa fedha nyingi zinazolipwa kama riba ya kuchelewa kutekeleza mikataba kwa wakati na kuziba mianya ya wizi kwa utitiri wa miradi isiyojulikana itakamilika lini.”

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments