Recent-Post

China yakabidhi EAC magari ya Sh 956 milioni

 

Serikali ya China imetoa msaada wa magari manane yenye thamani dola 400,000 (Sh 956 milioni) kwa uongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa ajili ya kurahisisha na kuboresha huduma.

Magari hayo yakiwemo mabasi matatu na magari madogo matano aina ya pick-up yenye thamani ya zaidi ya Sh900 milioni, yamekabidhiwa kwa uongozi wa jumuiya hiyo na ubalozi wa China nchini, Chen Mingjian jijini Arusha.

Akizungumza leo Juni 28 wakati wa kukabidhi magari hayo, Balozi Mingjian amesema kuwa msaada huo unalenga kuboresha na kukuza uhusiano na ushirikiano baina ya China na jumuiya hiyo.


"Magari haya yalikuwa yatolewe mwaka 2021 lakini kutokana na janga la Uviko-19 ndio maana limefanyika mwaka huu, ambayo hata hivyo bado sio mbaya maana uhitaji upo," amesema.

Amesema Serikali ya watu wa China imekuwa ikishirikiana na nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki katika masuala mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu wa sekta tofauti tofauti pamoja na kusaidia kukuza demokrasia, uwajibikaji na utawala bora.

"Tumekuwa tunasaidia katika nyanja mbalimbali kwa lengo la kukuza Amani, demokrasia na utawala bora pia uwajibikaji utakaosaidia jamii ya watu wa Afrika Mashariki kupata huduma bora na hatutaishia hapa bali tutaendelea kuhakikisha changamoto za EAC ni zetu pia," amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa sekta ya maendeleo ya Jamii, Irene Isaka aliyeokea magari hayo akimwakilisha Katibu mkuu wa EAC, amesema yatasaidia zaidi sekta ya michezo na mafunzo, semina na warsha kwa nchi wanachama.

"Magari haya ni matokeo ya mashirikiano mazuri baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Serikali ya watu wa China katika kukuza mtangamano wetu hivyo tunatoa shukrani zetu za dhati kwao," amesema.

Post a Comment

0 Comments