DC SIMANJIRO DKT SERERA AKABIDHI MADAWATI 50 SHULE YA ENDIAMTU

 MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dkt Suleiman Hassan Serera, amekabidhi madawati 50 kwa ajili ya kutumiwa na wanafunzi wa shule ya msingi Endiamtu, mji mdogo wa Mirerani, ambao wanaupungu wa madawati.


Dkt Serera amesema amekabidhi madawati hayo 50 baada ya kukuta kuna changamoto ya madawati hivyo akaonana na wadau wa maendeleo walioamua kusaidia wanafunzi hao.
 
“Madawati haya 50 yatapunguza tatizo la uchache wa madawati kwa wanafunzi wa shule ya msingi Endiamtu baada ya kusikia changamoto ya madawati,” amesema Dkt Serera.

Hata hivyo, amewataka wenyeviti wa vitongoji wa eneo hilo kupitia mikutano ya hadhara ya jamii kuangalia namna ya kuweza kujitoa na kuchangia hilo ili kumaliza tatizo la hilo.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Evetha Kyara amemshukuru Dkt Serera kuwapatia madawati hayo kwani wameingia asilimia 71 ya mafanikio kutoka asilimia 56 na kubaki asilimia 21.

Kyara amesema madawati hayo 50 yaliyotolewa na Dkt Serera yatatumiwa na wanafunzi 150 hivyo kupunguza tatizo hilo kwani baadhi ya madarasa, dawati moja wanakaa watoto watano.

Amesema shule ya msingi Endiamtu ina wanafunzi 981 wakiwemo wavulana 505 na wasichana 476, ikiwa na mahitaji ya madawati 350 yaliyopo ni 258 na pungufu ni 102.

Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo amemshukuru Dkt Serera kwa kufanikisha upatikanaji wa madawati hayo kwani yataondoa upungufu shuleni hapo.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukuteua kuja Simanjiro kwani umekuwa mchapakazi na pia kuipenda jamii, umeona changamoto ya madawati na kuifanyia kazi,” amesema Kobelo.

Amesema Dkt Serera amekuwa na upendo mkubwa na Mirerani ndiyo sababu ilipotokea changamoto ya upungufu wa madawati akaingilia kati na kutafuta wadau.

“Mkuu tunakushukuru mno kwani umekuwa ukiujali mji wetu mdogo wa Mirerani kuliko maeneo mengine ya Simanjiro hivyo tunaomba upendo huu uendelee kudumu,” amesema Kobelo.

Kiranja mkuu wa shule hiyo Mayege Masanja amemshukuru Mkuu huyo wa Wilaya ya Simanjiro Dkt Suleiman Hassan Serera kwa kuwakabidhi madawati hayo 50 kwao.

“Tunashukuru mno kwa kutupatia madawati haya kwani kwa namna moja au nyingine itapunguza mrundikano wa watoto watano hadi sita kukaa kwenye dawati moja badala ya dawati moja watoto,” amesema Masanja.

Mwanafunzi mwingine Husna Idd ametoa ombi kwa mkuu wa wilaya hiyo kuwapa kipaumbele kwenye ajira mpya ya walimu kwa kuipangia shule hiyo kwani wana upungufu wa walimu.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments