Viongozi wa dini ya kiislamu wamewaasa wazazi na walezi kusimamia maadili mema na malezi ya watoto ili kuwaepushae kuingia kwenye vishawishi vinavyopingana na maadili ya dini hiyo.
Hayo yamebainishwa na Sheikh Mikidadi Lipena kutoka Msikiti wa Mohamed Bin Ibrahim mkoani Dar es Salaam, wakati wa ibada ya swala ya Eid El Haji iliyofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Forest Hall leo Juni 28, 2023.
Sheikh Lipena amesema baadhi ya mataifa ya magharibi yamekuwa yakishawishi na kuhalalisha ndoa za jinsia moja kwa kigezo za usawa jambo ambalo ni kinyume na maadili ya dini ya kiislamu.
“Jamii ya kiislam na umma wa Watanzania wasikubali vishawishi vya kupata misaada, hivyo wazazi na walezi wafundishe watoto maadili mema ya dini, ambayo yanazuia kupingana na miongozo ya dini yetu ya kiislamu.” amesema.
Mwanafunzi wa mwaka wa tatu kozi ya ualimu Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro, Ummukuluthum Massanah, amesema njia ya kuwanusuru watoto kujiepusha na vitendo vinavyopingana na imani ya dini ni wazazi na walezi kuwafundisha watoto elimu ya dini ambayo ni silaha ya kupingana na vitendo viovu.
“Wazazi wana jukumu la kuwapatia elimu ya dini zao watoto ili wawe na utambuzi wa lipi jambo baya na zuri na kutambua haki zao. Binafsi naona hii ndio moja ya njia ya kuwajengea watoto uelewa na wale ambao uelewa bado ni mdogo wazazi wasiakae nao mbali,” amesema Ummukuluthum.
Akitoa salamu za Eid El Haji, Mwenyekiti wa Taasisi ya Islamic Foundation Tanzania, Arif Nahd amesema Serikali iingilie kati mmomonyoko wa maadili, kwa kuzipa nguvu za ziada taasisi za dini katika kusimamia maadili.
0 Comments