Dirisha moja la malipo kwa wafanyabiashara mbioni

 Kilio cha wafanyabiashara cha kuwapo kwa taasisi nyingi zinazohusika na kukusanya ada, tozo na adhabu kinaelekea kupatiwa dawa baada ya Serikali kupendekeza mfumo wa pamoja wa kufanya shughuli husika.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha Bungeni jijini Dodoma mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Utaratibu huo pia unaelezwa utasaidia taasisi za udhibiti kuweka utaratibu mzuri wa ukaguzi ambao hautasababisha usumbufu kwa wafanyabiashara.


Kuanza kwa mfumo huo pia kumetajwa kuwa utendaji kazi wake hautaathiri majukumu ya msingi ya taasisi hizo.

Pendekezo hilo la Serikali litakuwa ahueni kwa wafanyabiashara ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia kuwapo kwa taasisi nyingi za udhibiti wa biashara ambazo wakati mwingine zimekuwa zikikwamisha utendaji kazi wao kutokana na kupokea wageni wengi.

Dk Nchemba amesema pamoja na jitihada mbalimbali ikiwemo kufanya maboresho ya sheria ili kupunguza mwingiliano wa majukumu baina ya taasisi za udhibiti nchini na kufuta au kupunguza ada na tozo kero bado kumekuwa na changamoto.

Changamoto hiyo ni uwepo wa taasisi nyingi za udhibiti na usimamizi hali inayoongeza kero za ufanyaji wa biashara na uwekezaji ikiwemo kukosekana kwa mfumo mmoja wa ulipaji ada na tozo,  kuwepo kwa viwango vikubwa vya adhabu ambavyo hutumika kama vyanzo vya mapato.

Pia ametaja uwepo wa kaguzi nyingi zisizokuwa na tija, hivyo kuongeza usumbufu katika kufanya biashara.

“Serikali imeendelea kupokea malalamiko kutoka kwa wawekezaji na wafanyabiashara kuhusu kuongezeka kwa gharama za uzalishaji, uwekezaji na ufanyaji wa biashara nchini,” amesema Dk Nchemba.

Amesema uzoefu umeonyesha kuwa kaguzi nyingi zimekuwa zikifanyika kwa lengo la kutafuta makosa badala ya kuzuia kutokea kwa athari hasi.


“Pia adhabu kubwa zinazotolewa zinasababisha biashara kufanyika kwa hasara, ukubwa wa adhabu unaotoa fursa ya majadiliano kati ya watendaji na wafanyabiashara na hivyo kuipotezea Serikali mapato,” amesema

Amesema wakati mwingine adhabu hutumika kama motisha na chanzo cha mapato ya taasisi za udhibiti, na utitiri wa tozo, ada na adhabu na kutokuwepo kwa mfumo jumuishi wa kuzilipa.

“Katika kutatua kero hizo napendekeza kuanza matumizi ya mfumo wa pamoja wa ukusanyaji wa ada, tozo na adhabu za taasisi za udhibiti na taasisi za udhibiti kuweka utaratibu mzuri wa ukaguzi ambao hautasababisha usumbufu kwa wafanyabiashara bila kuathiri majukumu ya msingi ya taasisi hizo. Napendekeza hatua hizo zianze mwaka wa fedha 2023/24.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments