Dk Tulia aagiza hatua kwa waajiri wasiopeleka michango ya wafanyakazi

 Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameiagiza Serikali kuchukua hatua kwa waajiri wasiopeleka michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ili kuondoa usumbufu kwa wastaafu wakati wanapofuatilia stahiki zao.

Dk Tulia ameyasema hayo leo Jumatatu Juni 19, 2023 wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni.

Agizo hilo lilitokana na majibu ya Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, (CCM) Angelina Malembeka.


Malembeka alihoji Serikali imejipangaje katika kuhakikisha kuwa wastaafu wanapata mafao yao kwa wakati ikiwemo wastaafu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Akijibu swali hilo, Katambi amesema wastaafu wengi wamekuwa wakipokea taarifa kupitia simu ya kiganjani na yeyote ambaye anakuwa amecheleweshewa kupata mafao yake wamekuwa wakichukua hatua.

“Hasa katika kuhakikisha kwamba tunapata nyaraka zao sahihi na kwa wakati, ili waweze kulipwa. Kwa hiyo wachache sana ambao wanapata changamoto hizo kwa sasa na ikitokea tuna dawati maalum la kupokea changamoto hizo,”amesema.

Amesema kama zipo changamoto hizo anamuomba mbunge awafikishie taarifa ikiwa ni pamoja na za ATCL.

Amesema taarifa tulizonazo ofisini wameshalipwa zaidi ya wafanyakazi 500 na wale wachache ambao wanachangamoto ilikuwa ni kuhusiana na taarifa sahihi kutowasilishwa ofisini ili walipwe.

Hatua hiyo, ilimuibua Dk Tulia ambaye alisema suala la ucheleweshaji wa stahiki za wastaafu ni changamoto kubwa kwa wapigakura.

“Mmelipunguza kwa sehemu kubwa lakini bado ni changamoto wanapokwenda huko (mifuko) badala ya kuwalipa fedha unawaambia akafuatilie mwajiri wake kule wakati kazi ya kufuatilia siyo ya mwajiriwa kwa sababu yeye hawezi kuuliza kama umepeleka au hujapeleka,”amesema.


Amesema ni kazi ya yule mwenye mfuko ama ni kazi ya mfuko kufuatilia kwa yule ambaye halipi na kuwataka waendelee kulifuatilia upande wa mifuko iwapo waajiri wanapeleka michango.

“Kama hawapeleki ichukulieni hatua mifuko lakini huyu mwajiriwa asipate tabu anapostaafu alipwe pesa yake,”amesema.

Akijibu Katambi amesema mifuko ina sheria ambazo zinaanzishwa zinazoeleza kuwa ni kosa kwa mwajiri kutokuwasilisha michango kwa wakati katika mifuko hiyo kwa ajili ya wanachama.

Amesema ikitokea hivyo hata mahakamani wanawapeleka kwa sababu Bunge lilitunga sheria ya kutambua umuhimu wa watu hao.

“Unapelekwa mahakamani hakuna kujitetea na sisi tunachukua hatua, hivyo kama kuna maeneo ambayo watakuwa wamechelewesha michango nitoe rai kupitia Bunge hili kwamba tunawataka waajiri wote nchini kutekeleza hilo,”amesema.

Ameitaka waajiri kupeleka michango ya wanachama kwa wakati ili wasisumbuke, na kuipunguzia Serikali mashauri yaliyopo mahakamani maana hadi sasa yapo zaidi ya 26 na hatua zimechukuliwa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments