Giza latanda uchaguzi makamu mwenyekiti CCM Simanjiro

Giza limetanda kwenye uchaguzi wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, kupitia CCM kuahirishwa kila mara.

Hadi leo Jumanne ya Juni 27 mwaka 2023, halmashauri nyingine sita za wilaya za mkoa huo zimeshafanya uchaguzi wao kupitia CCM na kupata wagombea wa nafasi hizo isipokuwa halmashauri ya Simanjiro.

Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Amos Shimba amethibitisha kuahirishwa kwa uchaguzi huo ambapo madiwani saba walichukua na kurejesha fomu za kugombea nafasi hiyo ya Makamu Mwenyekiti.


"Tumepata agizo kutoka CCM mkoa juu ya kusitisha kwa muda uchaguzi huo hivyo tunasubiria maelekezo mengine kisha tutawapa mrejesho," amesema Shimba.

Amewataja waliochukua na kurejesha fomu ya kugombea nafasi hiyo ni makamu mwenyekiti anayemaliza muda wake, Jacob Kimeso ambaye ni diwani wa kata ya Edonyongijape na diwani wa kata ya Ngorika Albert Msole.

Amewataja madiwani wengine na kata zao kwenye mabano ni Lucas Zacharia (Endiamtu), Salome Mnyawi (Mirerani), Sendeu Laizer (Orkesumet), Kaleiya Mollel (Msitu wa Tembo) na Yohana Shinini (Emboreet).

Mmoja kati ya wagombea wa nafasi hiyo ambaye hakupenda kutaja jina lake, amesema CCM wilaya walishatimiza wajibu wao ila CCM ngazi ya mkoa ndiyo wanakwamisha.

"CCM wilaya ya Simanjiro walipeleka majina yote saba na kupendekeza majina matatu ya kurudishwa ila CCM mkoa wakarudisha majina yote saba," amesema.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer alipoulizwa juu ya sintofahamu ya kuahirishwa kila mara kufanyika uchaguzi huo amesema CCM ngazi ya mkoa ndiyo wenye majibu.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Peter Toima amesema watatoa utaratibu wa uchaguzi wa nafasi hiyo kwa wilaya ya Simanjiro.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments