Chongolo amesema kukamilika kwa uwanja huo kutaongeza fursa za utalii na kiuchumi kwa mji wa Iringa na mikoa ya nyanda za juu Kusini.
Pia ameshauri kujengwa kwa kituo kitakachosaidia kuhifadhi historia ya makabila ya kusini.
Chongolo ametoa ushauri huo baada ya kukagua Uwanja wa Ndege wa Iringa ambao upo kwenye hatua ya ujenzi.
Amesema kwa sababu uwanja huo utafungua utalii wa kusini ni muhimu mkakati wa kuwa na makumbusho ukawepo.
"Inabidi muwe na boma lenye historia ya makabila ya kusini, tujenge tabia ya kurithisha tamaduni zetu," amesema Chongolo.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amesema tayari mkoa huo ni kitovu cha utalii wa kusini mwa Tanzania.
Hata hivyo amesema awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo itakuwa ni kuongeza urefu wa barabara ya kutulia ndege ikiwamo za mizigo.
"Mkoa wa Iringa ni kitovu na lango la utalii wa kusini mwa Tanzania, kwa sababu uwanja unahitaji eneo kubwa zaidi, mikakati inaendelea," amesema.
Awali, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Baptista Nyengo amesema jumla ya Sh2.8 bilioni zimelipwa kwa wananchi 234 kama fidia ya maeneo yao.
0 Comments