Kauli tata za viongozi zaibua mjadala nchini

Ulimi ni kiungo kidogo na laini, lakini matokeo yake huwa na faida au hasara kubwa kulingana na kile kilichotamkwa.

Hivi karibuni viongozi wametoa kauli zilizosababisha kuibuka kwa hisia za ubaguzi, ubabe na dharau kwenye jamii.

Miongoni mwa kauli hizo ni ile aliyoitoa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo kuwa Katiba mpya itatengenezwa kupitia mikono ya chama hicho.

Kauli hiyo aliyoitoa akiwa ziarani mkoani Iringa, imeibua malalamiko hasa kwa vyama vya upinzani, ambavyo vimekuwa mstari wa mbele katika kudai mabadiliko ya Katiba yatakayogusa na kushirikisha wananchi wengi.


Tayari chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinachoendelea na mazungumzo ya maridhiano ya kisiasa na CCM, kimeshaweka msimamo kuwa bila Katiba mpya, hawatashiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 na uchaguzi mkuu.

Kauli ya Chongolo juu ya Katiba mpya na zile za Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu na Katibu mkuu wake, John Mnyika za kususia uchaguzi kama hakuna Katiba mpya ni dalili hali si shwari katika maridhiano hayo.

Kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila iliyotafsiriwa kuwatumia viongozi wa dini kumnyooshea njia Rais Samia Suluhu kuelekea 2025 nayo imeibua mjadala.

Chalamila, aliyetoa kauli hiyo mbele ya Rais wakati wa kupokea ndege mpya ya mizigo Boeing B767-300F jijini Dar es Salaam, ni kama zimewasha moto wa Katiba na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
 

Walichokisema Chongolo, Chalamila

Akizungumza katika ziara mkoani Iringa wiki iliyopita, Chongolo alisema kuna jambo la Katiba mpya na kwamba kuna watu wanapigapiga kelele ambao hata hivyo hakuwataja, lakini akataka wana CCM waelewe CCM ndiyo kitaratibu mchakato.

“CCM ndiyo chama kiongozi na ndiyo chama kitakachoongoza mchakato wa Katiba ya kisasa. Katiba iliyopitiwa na kuandaliwa kisasa, itatengenezwa kwa mikono na uongozi na usimamizi na uratibu wa CCM na siyo vinginevyo,” alisema Chongolo.

“Msidanganyike. Watu wengi wanalalamikia na kutaka Katiba kwa masilahi binafsi. Wengi ukiangalia kwenye Katiba mpya hawazungumzii pembejeo za kilimo, hawazungumzii uhakika wa usalama wa Watanzania, miundombinu ya barabara.

“Wanazungumzia wanataka Tume huru ya uchaguzi, wanataka mambo yatayowapa nafasi ya kwenda kwenye madaraka. Lazima tuangalie mambo yanayokwenda kuboresha maisha ya Watanzania kutokea hapa kwenda mbele,” alisema.

Kwa upande wake, Chalamila alimwaga takwimu za fedha ambazo zilizotolewa na Serikali kwa Jiji la Dar es Salaam, akisema hizo ni cheche tu ili kuwatisha wale wanaowabishia.

“Lakini (mheshimiwa Rais) hapa Dar es Salaam kwa wiki lijalo (wiki hii) nitakuwa na kikao na viongozi wa dini. Agenda kubwa ni tokomeza adui ili Rais Samia apenye bila kupingwa,” alisema Chalamila, kauli inayohusishwa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwenye kikao cha viongozi wa dini na Chalamilka kilichofanyika Juni 7, mwaka huu, zilibainisha kuwa kiongozi huyo alitumia mkutano huo kumpongeza Rais kwa miradi iliyotekelezwa katika Jiji la Dar es Salaam na kuahidi kushirikiana na viongozi wa dini, hivyo ajenda hiyo haikuwapo.
 

Viongozi wa dini wanena

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo, alisema kauli hizo zinaweza kuzua mtafuruku usio na sababu, huku akionya viongozi wa dini waepuke kutumika kisiasa au kwa masilahi ya kundi fulani.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, alisema mchakato wa Katiba mpya utasimamiwa na sheria itakayotungwa na Bunge, akihoji kauli ya Chongolo ameitoa kwa sheria ipi.


Askofu Shoo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), alisema haelewi dhamira za viongozi hao zilikuwa nini hadi waliamua kuzitoa, lakini ni za hatari na zinaweza kuibua mtarafuku.

“Tena wajihadhari sana wasitumike kisiasa kwa masilahi ya kundi fulani,” alisisitiza Askofu Shoo.
Padri Kitima alisema hadhani kama Chalamila alitumwa na Serikali kusema aliyoyasema, lakini kwa kauli ya Chongolo anaweza kusema alichokisema.

“Kuna sheria lazima itengenezwe ndiyo iweke utaratibu na katika kutunga sheria ni Bunge ambalo ni la wawakilishi wa wananchi ndio wanaotengeneza sheria ya utaratibu mzima utakaofuatwa katika kutengeneza Katiba.

“Tuseme kwa ujumla mchakato wa kutengeneza Katiba utatokana na sheria ya nchi, wala siyo kusema kwamba ni chama fulani. Kama watakuja na sheria mpya ambayo inasema chama, basi tusubiri tuone, mpaka sasa hatuwezi kutoa hukumu,” alisema.

Padri Kitima alisema: “Katiba tunayoitafuta siyo ya vyama vya siasa, ni Katiba ya wananchi wa Tanzania namna wanavyotaka kujiongoza na kujitawala katika nchi yao,” alisisitiza Padri Kitima na kuongeza kuwa ni lazima mchakato uongozwe na sheria.

Kuhusu Chalamila, alisema ana haki ya kuwakutanisha viongozi wa dini ili kumsaidia kudumisha amani katika mkoa, na masuala ya kukutana ili kujadili ajenda ya kumsaidia kiongozi katika uchaguzi mkuu siyo wajibu wao.

“Kuhusu mkutano wa viongozi wa dini na uchaguzi wa 2025 hilo siyo suala ambalo sisi linatuhusu. Mambo ya uchaguzi yapo nje ya suala la kutukutanisha sisi. Sisi akitukutanisha siyo suala la kuongelea uchaguzi au nini. Ni amani,” alisema.


Kwa upande wake Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda Issa alisema suala la kuanzisha mchakato wa Katiba siyo la chama fulani, bali ni la Watanzania.

Alisema hivi sasa suala siyo kujadili Katiba mpya, bali utekelezaji wake, akiwataka viongozi kutotoa kauli zitakazovuruga mchakato huo.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga akizungumzia kauli ya Chongolo, alisema ili Tanzania iwe na Katiba mpya yenye uhalali ni kuwa na Katiba iliyohusisha makundi yote.

Wakili na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Ruaha (Rucu) mkoani Iringa, Dk Rwezara Kaijage aliwataka Watanzania kupima kauli za kina Chongolo, Chalamila na viongozi wengine wa kisiasa kabla ya kuzibeba, kuziamini na kuziishi.

“Kauli kama hizo zinatolewa na viongozi si kwa minajili ya kuwaburuza Watanzania, bali kila kiongozi anapalilia au kuimarisha alipo. Ni juu ya wananchi kupima na kuchagua kati ya mbivu na mbichi,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe alisema kauli ya Chongolo inaendelea kuwakumbusha wananchi kuamka ili kupigania hatima ya maisha yao kupitia Katiba mpya na siyo kuwaachia wanasiasa pekee.

“Watanzania lazima wawe mstari wa mbele katika mchakato wa Katiba mpya kwa sababu tofauti yao na wanasiasa ni kwamba, wao wanapigania hatima ya maisha yao, lakini wanasiasa wanapigania madaraka.

“Ni muhimu sasa yafanyike mabadiliko ya sheria za kuratibu mchakato ambayo pamoja na mambo mengine yataelekeza uundwaji wa kamati ya wataalamu na vigezo vya kuwapata ili kamati hiyo itengeneze rasimu ya Katiba pendekezwa,” alisema.

Msimamo vyama vya siasa

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema kauli za viongozi hao wawili zinaligawa taifa badala ya kuliunganisha.

“Wakati Rais Samia alipokuwa anamjibu Mwenyekiti Mbowe (Freeman) kwenye siku ya maadhimisho ya wanawake duniani alisema kuhusu wahafidhina wa kupinga Katiba mpya na maridhiano. Huu (wa Chongolo) ndiyo ushahidi wenyewe.”

Mrema alisema watu wa aina hiyo hawakosekani katika jamii, lakini anaamini nguvu ya umma itashinda katika jambo hilo. Alisema kauli hizo hazijatolewa kwa bahati mbaya, ila zina lengo la kufifisha mapambano ya kudai Katiba mpya.

“Ushauri wangu, wamsikilize mwenyekiti wao na wasome alama za nyakati. Tumeshatoka zama za giza na kamwe hatutarudi huko tena. Wakumbuke kauli hii ilitoka kinywani mwa Rais pale Moshi siku ya wanawake duniani. Waitafakari,” alisema.

Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alisema kauli ya Chongolo kuhusu mchakato wa Katiba mpya siyo sahihi.
“Mchakato wa Katiba mpya hauratibiwi na chama chochote cha siasa. Ni mchakato wa kitaifa uliopaswa kuratibiwa kwa muafaka wa kitaifa na Watanzania wote. Lazima ushirikishe makundi yote muhimu kwenye jamii.
 

Kauli ya Mbowe

Kwa upande mwingine, Juni 7 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitoa msimamo wa chama chake kuhusu makubaliano ya ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai juu ya uboreshaji na uendeshaji wa bandari Tanzania.

Katika maelezo yake, Mbowe alisema: “Je, kama kweli mkataba huu una manufaa makubwa kwa nchi yetu kama inavyodaiwa na CCM na wapambe wake, kwa nini bandari ya Zanzibar haimo kwenye mkataba huu?


“Kwa msingi huo na katika mazingira haya, Watanganyika wana haki ya kuhisi kwamba Wazanzibari hawa wawili wanagawana mali za Tanganyika kwa wageni kwa faida zao binafsi, wakati wakilinda mali zao wenyewe katika nchi yao ya Zanzibar,” alisema.

Kauli hiyo imeibua mijadala, hasa kwa wanaounga mkono uwekezaji na uboreshaji wa bandari, akiwamo Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde aliyewaambia waandishi wa habari juzi jijini Dodoma kuwa kauli hiyo ni ya kibaguzi.

“Mbowe anayesema Rais na Waziri wanaotoka Zanzibar, ila bandari ni ya Dar es Salaam. Hii inaweza ikaharibu Muungano, haya ni maneno yasiyo na uungwana, kwani anataka kutuaminisha ni kosa Rais na waziri kutoka Zanzibar. Huo ni ubaguzi.

“Hivi Rais akitoka Kilimanjaro mipaka yake ya kutoa uamuzi ihusu milima tu? Vitu vingine visiguswe, asizungumze kuhusu korosho azungumzie Kilimanjaro tu? Haiwezekani?” alisema Mbunge huyo.

Kwa upande mwingine, akizungumza kupitia taarifa iliyotolewa na chama cha ACT Wazalendo, kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe aliwataka Watanzania kujadili masuala haya kwa misingi ya ukweli bila kuweka hisia za kibaguzi. “Viongozi wa kisiasa tuwe makini na kauli tunazotoa, kwani zinaweza kuongeza taharuki kwenye masuala ambayo kwa hakika yanahitaji ‘ukweli’ kuliko hisia,” alisema.TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments