MADIWANI SABA SIMANJIRO WAJITOSA KUGOMBEA UMAKAMU MWENYEKITI

Madiwani  saba wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, kupitia CCM wameomba kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Simanjiro, Amos Shimba amethibitisha madiwani hao saba kuchukua na kurejesha fomu za kugombea nafasi hiyo ya Makamu Mwenyekiti.

Shimba amewataja waliorejesha fomu ni makamu mwenyekiti anayemaliza muda wake, Jacob Kimeso ambaye ni diwani wa kata ya Edonyongijape na diwani wa kata ya Ngorika Albert Msole.

Amewataja madiwani wengine na kata zao kwenye mabano ni Lucas Chimba Zacharia (Endiamtu), Salome Nelson Mnyawi (Mirerani), Sendeu Laizer (Orkesumet), Kaleiya Mollel (Msitu wa Tembo) na Yohana Shinini (Emboreet).

Amesema utaratibu wa nafasi ya makamu mwenyekiti wa halmashauri ni muda wa mwaka mmoja hivyo Juni 30 ndiyo mwisho hivyo uchaguzi unapaswa kufanyika upya.

“Kamati ya siasa ya wilaya imeshafanya mchakato wake hivyo tumepeleka majina yote saba kwenye ngazi ya mkoa ili majina matatu yarejeshwe ili yaje kupigiwa kura,” amesema Shimba.

Amesema madiwani wa halmashauri hiyo wanapaswa kuchagua jina moja kati ya majina matatu pindi yakirejeshwa na CCM ngazi ya mkoa hivyo wajiandae kwa hilo.

“Madiwani wote wa Simanjiro ni kupitia CCM hivyo wanapaswa kuwa watulivu kwenye kipindi hiki kwani wataelezwa namna ya utaratibu wa kupiga kura,” amesema Shimba.

Madiwani wa kata ya Ngorika, Albert Msole na kata ya Orkesumet, Sendeu Laizer wamethibitisha kuchukua fomu za kugombea na wanasubiria uamuzi wa chama chao.

Madiwani wa kata ya Mirerani, Salome Nelson Mnyawi na kata ya Endiamtu, Lucas Chimba Zacharia wamesema wamechukua fomu za kugombea nafasi hiyo ila wanasubiri utaratibu wa CCM. 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments