Mbunge Mnyeti alia vifaa tiba, Rais Samia atoa majibu

Mbunge wa Misungwi, Alexander Mnyeti ameiomba Serikali kupeleka vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi kuwezesha wananchi kupata huduma bora za afya.

Akitoa salaam kwa niaba ya wapiga kura wake leo Juni 14, 2023, wakati wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa daraja la JPM maarufu kama daraja la Kigongo-Busisi inayounganisha Wilaya za Misungwi na Sengerema, Mnyeti amesema gharama ya vifaa tiba vinavyohitajika ni zaidi ya Sh500 milioni.

“Rais Samia, Serikali imetupatia Wilaya ya Misungwi zaidi ya Sh3 bilioni kwa ajili ya miradi ya afya; ujenzi wa Hospitali ya wilaya imekamilika, sasa tunaomba Sh500 milioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba ili wananchi waanze kunufaika na utekelezaji wa mradi huu,” amesema Mnyeti.


Akijibu ombi hilo, Rais Samia ameahidi kuwa Serikali itanunua vifaa tiba kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Misungwi kama inavyofanya katika wilaya na maeneo mengine nchini kutekeleza mikakati ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

“Mbunge amesema kuhusu suala la Hospitali ya Wilaya ya Misungwi, nataka niwambie vifaa tiba vinakuja na hatutaacha kifaa hata kimoja kinachopaswa kuwepo katika ngazi ya wilaya. Nawaahidi Serikali yenu itafanyia kazi suala hili,” amesema Rais Samia na kuamsha shangwe kutoka kwa wananchi waliokuwa wanamsikiliza eneo la kivuko cha Kigongo-Busisi.

Mkuu huyo wan chi amewaomba Watanzania popote walipo kuendelea kushirikiana na kuiunga mkono juhudi za Serikali za kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Akizungumzia utekelezaji wa ujenzi wa daraja la JPM, Amiri Jeshi Mkuu huyo amewasihi vijana na wataalam wa Kitanzania waliopata fursa za ajira katika madi huo kujifunza na kupata ujuzi kutoka kwa wataalam wa kigeni ili baadaye waweze kusaidia Taifa katika utekelezaji wa miradi ya aina hiyo siku zijazo.


Huku akionya kuhusu tabia ya udokozi na wizi wa vifaa, Rais Samia amesema; “Wale wenye mikono mirefu ya kudokoa saruji na vifaa vya ujenzi waache kwa sababu mradi huu ni wetu sote; kukamilika kwake ni manufaa kwetu sote,”

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments