Mfupa uliomshinda fisi akabidhiwa Chongolo

HALMASHAURI ya Manispaa ya Iringa imempigia magoti Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ikiomba awasaidie kuisukuma serikali itoe Sh bilioni 1.9 zinazohitajika kukamilisha miundombinu ya machinjio ya kisasa.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Gwanda alisema miundombinu hiyo inahusisha mashine za kisasa za kuchinjia na kupoozea. Ombi hili limetolewa leo baada ya mtendaji huyo mkuu wa chama tawala kutembela mradi huo kwa lengo la kujionea maendeleo na changamoto zake.

Awali Ofisa Mifugo na Uvuvi wa Manispaa hiyo, Dk Steven Ngwale alisema pamoja na ukosefu wa mashine hizo, machinjio hiyo iliyokamilika kwa asilimia 95 imeanza kufanya kazi toka Julai, mwaka jana.

“Kwa kuwa hatuna vifaa hivyo tunalazimika kuchinja kwa njia ya kawaida kwa wastani wa ng’ombe 45, mbuzi 40 na kondoo chini 40 kwa siku jambo linaloipotezea sifa ya machinjio ya kisasa na hata makusanyo yake ” alisema.

Alisema tangu ianze kazi Julai mwaka jana machinjio hiyo imeweza kukusanya ushuru wa machinjio wa Sh Milioni 60.6 tu, kiwango ambacho ni kidogo kama ingekuwa imekamilika.

Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Jessa Msambatavangu alipigilia zaidi maombi ya fedha hizo akisema wanazihitaji ili kuifanya machinjio hiyo kupata hadhi ya kuwa kiwanda cha nyama zitakazikuwa zikiuzwa hadi nje ya mkoa na nchi.

“Badala ya kuchinja mbuzi 35 au 40 kwa siku ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuchinja mbuzi 500 kwa siku jambo litakaloongeza mnyololo wa thamani katika sekta ya mifugo,” alitoa mfano.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego alisema mradi huo umegeuka kuwa kero kwasababu kutokamilika kwake kumeufanya uongeze gharama kwa serikali.

Akijibu maombi hayo, Chongolo aliahidi kuiagiza Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuufuatilia mradi huo kabla hajakutana na mamlaka zingine zinazotakiwa katika kikao atakachokiitisha jijini Didoma kwa kumuhusisha Mkuu wa Mkoa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa.

Awali Chongolo katika ziara yake ya siku sita mkoani Iringa anayohitimisha leo mjini Iringa ametembelea ukarabati wa uwanja wa ndege wa Iringa ambao awali ulikuwa ukamilike Agosti mwaka huu.

Kaimu Meneja wa Tanroads Mkoa wa Iringa, Batista Nyengo alisema uwanja huo unaokarabatiwa kwa zaidi ya Sh Bilioni 61 utakamilika Oktoba mwaka huu.

“Mpaka sasa ukarabati wa jumla umefikia asilimia 54.8 na mkandarasi amekwishalipwa zaidi ya Sh bilioni 24 kati ya Sh bilioni 29 alizoomba,” alisema.

Chongolo alisema kukamilika kwa uwanja huo kutachochea shughuli za utalii, kilimo na usafirishaji wa abiria na hivyo kukuza uchumi wa wana Iringa na Taifa kwa ujumla.

“Wajibu wenu kama wana Iringa ni kujiunganisha na biashara na masoko yatakayotuletea zaidi fedha za kigeni. Mna ardhi nzuri sana kwa kilimo cha mbogamboga zenye soko kubwa na la uhakika ndani na nje ya nchi,” alisema.

Wakati awamu ya kwanza ya ukarabati huo ikielekea kukamilika Mkuu wa Mkoa amesema wanaendelea na mazungumzo na mradi wa Regrow kwa lengo la kuupanua zaidi uwanja huo utakaokuwa na uwezo wa kupokea ndege za ukubwa wa Bombardier ili upokee ndege kubwa zaidi zikiwemo za mizigo.

Katika ziara hiyo Chongolo ametembelea pia mradi wa barabara ya mchepuo ya Tumaini Igumbilo na kushauri ijengwe kwa kiwango cha changarawe wakati Sh bilioni 18 zinazohitajika kwa ajili ya kiwango cha lami zikiendelea kutafutwa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments