Mifugo 2,600 ‘wadondoka’ Mirerani, ni katika kusherehekea Eid Al adha


Taasisi mbalimbali ikihusisha wajane, wagane, na yatima wilayani hapa, wamepata mgao wa nyama baada ya ngombe 600, mbuzi na kondoo 2,000 kuchinjwa katika ikiwa ni ishara ya kusherehekea sikukuu ya Eid Al adha.

Mwenyekiti wa taasisi ya Ahasante Foundation Tanzania, Katada Kimaro akizungumza leo alhamisi Juni 29 2023 amesema mifugo hiyo imechinjwa kwa lengo la kutolewa sadaka kwa wahitaji.

Kimaro amesema taasisi hiyo pia imechinga mifugo kwenye maeneo tofauti ikiwemo Kata ya Makiba wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha ambapo ng'ombe 50 na mbuzi 200 wamechinjwa; huku Kata ya Mirongoine mkoani Singida wakichinjwa ng'ombe 150.


Amesema taasisi hiyo imefanikisha tukio hilo kwa kushirikiana na taasisi ya Paylas Kurbanini Kurban 2023 ya kutoka nchi ya Uturuki.

"Walengwa hasa ni wale wahitaji ikiwemo wajane, wagane, yatima, wagonjwa na wenye mahitaji mbalimbali ikiwemo taasisi za binafsi na za serikali kama vile vituo vya afya Mirerani," amesema Kimaro.

Mmoja kati ya wahitaji waliopata msaada huo Mariam Hamis amezishukuru taasisi hizo kwa kuwapatia kitoweo kwenye sikukuu hiyo.

"Hii ni sikukuu ya Eid Al adha ya kuchinja na mimi na wanangu tunapata kitoweo na kufurahia sherehe ya idi kama watu wengine wanavyofurahi," amesema

Kasim Omary ameishukuru taasisi hiyo kwa kugawa kitoweo kwa wahitaji mbalimbali hasa wanawake wajane, wagane, yatima na taasisi mbalimbali.

"Mwaka jana 2022 taasisi hii ilifanya hivi hivi kwa kusaidia jamii katika sikukuu ya idi tunawashukuru mno kwa kurudia tena mwaka huu," amesema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments