Mpaka Hifadhi ya Ruaha warekebishwa

SERIKALI imewasilisha rasmi bungeni Azimio la kurekebisha mpaka wa Hifadhi ya Taifa Ruaha. Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohammed Mchengerwa aliwasilisha azimio hilo jana likaungwa mkono na kupitishwa na Bunge.

Mchengerwa alisema pendekezo la marekebisho ya mipaka hiyo liliafikiwa kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika mkutano wa hadhara na wananchi uliofanyika Januari 18, mwaka huu katika eneo la Kapunga Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya.

Alisema mkutano huo ulipendekeza kurekebisha mpaka wa hifadhi hiyo kwa kuzingatia mapendekezo yaliyowasilishwa na kamati ya mawaziri wanane wa kisekta.

Mchengerwa alitaja fursa na manufaa ya kurekebisha mpaka huo kuwa ni kupatikana kwa eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 478 litakalomegwa kutoka sehemu ya hifadhi kwenda kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za kiuchumi kama vile kilimo na ufugaji katika vijiji 29.

Pia, alisema hatua hiyo itahifadhi vyanzo vya maji vilivyopo katika Bonde la Usangu na kuimarisha mtiririko wa maji kwenye milima ya Kipengere na Uporoto kuelekea lindimaji la Ihefu. Eneo hilo ni chanzo cha Mto Ruaha Mkuu unaotegemewa kuzalisha umeme wa maji katika mabwawa ya Mtera, Kidatu na Bwawa la Julius Nyerere ili kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini.

Mchengerwa alisema pia marekebisho hayo yataboresha mifumo ikolojia ya Bonde la Usangu ili kurejesha wanyamapori na uoto wa asili kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Alisema pia yataimarisha uhifadhi wa maliasili hasa wanyamapori, mimea, mazalia na makuzio ya samaki na viumbemaji wengine na kuondoa migogoro ya mipaka baina ya Hifadhi ya Taifa Ruaha na vijiji husika.

Alieleza kuwa pia yataongeza mchango wa pato la taifa kupitia utalii katika Hifadhi ya Taifa Ruaha na kuwezesha upatikanaji wa maji kwa ajili ya shughuli nyingine za kiuchumi kikiwemo kilimo, ufugaji na uvuvi.

“Kwa mujibu wa masharti ya nyongeza ya kifungu cha 4 cha Sheria ya Hifadhi za Taifa, Sura ya 282, Rais amepewa mamlaka ya kurekebisha mipaka ya eneo lolote lililotangazwa kuwa Hifadhi ya Taifa baada ya kupata idhini ya Bunge, na kwa Tamko litakalochapishwa kwenye Gazeti la Serikali,” alisema Mchengerwa.

Hifadhi ya Taifa Ruaha ilianzishwa kwa Tangazo la Serikali Namba 464 la Mwaka 1964 ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 10,300. Baadaye ilifanyiwa marekerebisho kupitia Tangazo la Serikali Namba 28 la Mwaka 2008 kwa kuongeza eneo la Bonde la Usangu na kufikia ukubwa wa kilomita za mraba 20,300.

Lengo la kuanzishwa kwa hifadhi lilikuwa ni kuhifadhi na kulinda bioanuai hasa wanyamapori, mimea, mazalia na makuzio ya samaki na mtiririko wa maji kwenye mto Ruaha Mkuu ambao ni chanzo kikuu cha maji kwenye mabwawa ya kufua umeme.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Timotheo Mnzava alisema ili kuwe na uhifadhi wenye tija kwa hifadhi ni lazima serikali ihakikishe migogoro ya mipaka kati ya maeneo ya ardhi za vijiji na maeneo yaliyohifadhiwa inapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Alisema kamati hiyo inapendekeza serikali iepuke uwezekano wa mpaka mpya wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kukabiliwa na migogoro dhidi ya vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments