Hayo yanathibishwa na baadhi ya wamiliki wa vyombo vya usafiri na watembea kwa miguu wanaodai maeneo mengi yaliyokuwa sugu kwa kujaa maji kipindi cha mvua kama Jangwani na Kamata yameendelea na hali hiyo jambo linaloleta kero kwao.
Mvua hizo zilizoanza kunyesha kuanzia alfajiri ya kuamkia leo Juni 5, 2023 zimeleta madhara mbalimbali kwa wakazi wa jiji hili ikiwemo kushindwa kufika kazini kwa wakati.
Wakizungumzia changamoto hizo watumiaji wa barabara jijini hapa wamedai licha ya kujengwa kwa lami zimekuwa zikijaa maji kiasi kwamba hata watumiaji wa vyombo vya usafiri wanaogopa kupita.
“Eneo la Kamata limekuwa sugu limekuwa likitusababishia vyombo vyetu kama hizi pikipiki kuharibika,’’ amesema Joseph Stanley ambaye ni dereva wa bodaboda eneo la Kamata.
Hoja hiyo imeungwa mkono na Charles Amos ambaye ni mkazi wa Kariakoo amesema afya zao zinakuwa hatarini kwasababu wanatembea kwenye barabara ambazo zimejaa maji ambayo hawajui yanatoka wapi.
“Kwa mfano hapa Kariakoo kuna watu wanazibua vyoo na kuviacha vitiririshe uchafu. Kwa sisi watembea kwa miguu tunapita katika maji haya tunakuwa hatarini kupata magonjwa kama fangasi,”amesema Amos
Issa Juma dereva wa daladala ameiomba serikali kuangalia namna ya kuwasaidia katika maeneo ambayo yamekuwa kero kipindi cha mvua kwani magari yao yanakuwa hatarini kuharibika.
“Maji yakijaa hadi kiwango fulani inakuwa shida kupitisha magari kwani yanaingia ndani ndiyo maana mnaona tunalazimika kupita maeneo mengine kuhofia kuipita sehemu zenye maji mengi kulinda vyombo vyetu,”amesema
Amesema barabara nyingi zimekuwa na mshimo makubwa na unakuta sehemu hiyo maji yamejaa hivyo inakuwa vigumu kupata ramani nzuri ya kupita na kujikuta imeingia kwenye shimo.
0 Comments