Mwigulu Ataka Wamiliki Ardhi Kunufaika.

                                 

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amewataka watendaji wa Serikali kutoa fursa kwa wamiliki wa ardhi kunufaika na maeneo wanayomiliki pale wawekezaji wanapohitaji ardhi kwa ajili ya kuwekeza nchini.

Amesema maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi hivyo ni lazima watendaji wote serikalini wawe na nidhamu ya kuilea na kuiwezesha sekta binafsi kukua na kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi badala ya kufanya urasimu na kuwadhibiti.


Dk Mwigulu ameyasema hayo leo bungeni wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambao amesema “Tunatumia nguvu kubwa kwenye kudhibiti kuliko nguvu tunayoitumia kuwezesha. Lazima tuheshimu sekta binafsi na kutambua mchango wake katika kutoa ajira, kuondoa umaskini na kukuza uchumi. Nitoe rai kwa Watanzania wenzangu tuwe na nidhamu katika kuiwezesha sekta binafsi kukua.

 “Hali ilivyo sasa, wawekezaji wa ndani wakijaribu kupiga hatua wanapigwa vita na kukatishwa tamaa. Hata wamiliki wa ardhi hawapati fidia stahiki pale wawekezaji wanapohitaji kumilikishwa ardhi hizo kana kwamba watanzania hawatakiwi kutajirika. Nitoe rai kwa watendaji wa Serikali, acheni Watanzania walipwe pesa nyingi, acheni Watanzania watajirike!

Dk Mwigulu amesema licha ya kwamba wawekezaji hao wanaleta mtaji, teknolojia, ajira, kuongeza mapato kwa Serikali na kukuza uchumi, uzoefu unaonyesha kuwa, wawekezaji hao wanakumbana na vikwazo kuliko uwezeshaji ndani ya Serikali na hata kwa wananchi.

“Jawabu la ukosefu wa ajira kwa vijana na kuondoa umaskini kwa Watanzania ni kukuza uwekezaji, hususan katika sekta za uzalishaji na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi,”amesema Dk Mwigulu.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments