Nape ataka wapotoshaji washughulikiwe

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape nnauye ametaka wote waliopotosha umma kuhusu suala la mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai, washughulikiwe ili wasiendelee kupotosha umma.

Nape ambaye pia ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amebainisha hayo leo Juni 10, 2023 wakati wa mjadala wa kupitisha azimio kuhusu pendekezo la kuridhiwa kwa mkataba baina ya serikali hizo kuhusu uendeshaji wa bandari nchini.

Mbunge huyo ameeleza hayo wakati kukiwa na mjadala mpana wa watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa, wanasheria na watu wa kawaida ambao wanaupinga mkataba huo kwa madai kwamba una upungufu unaotishia maslahi ya Taifa.


“Wapo watu wachache walitaka kutumia hofu hii kulikoroga Taifa na hawa tunatakiwa kushughulika nao kwa sababu mbegu hata kama ni ndogo namna gani ikipuuzwa iko siku itaota itaathiri taifa letu.

“Kwenye hili ni vizuri tusimung’unye maneno, hawa tuwakabili usoni mchana kweupe. Asilimia 90 ya Watanzania tulizaliwa baada ya muungano, hizi tofauti huko hatukuzikuta wala hatuzijui, zilishazikwa na Muungano,” amesema Nape.

“Sasa anatokea mtu mzima, anaaminika, tumempa heshima, na kati ya watu waliompa heshima ni Rais Samia. Rais huyu akasema twende kwenye maridhiano, kwa uungwana kabisa, hatukubadili katiba, leo kwa kulewa”

Ameongeza kwamba: “Sisi wana CCM ndiyo waasisi wa maridhiano, hatukulazimishwa na mtu, tunayaamini lakini maridhiano yasitumike kuligawa taifa letu, sisi hatutakubali. Hivi leo, Profesa Mbarawa, uzalendo wake, unakwenda kutwezwa kijinga tu, kilevi. Hapana.”

Nape amebainisha kwamba Watanzania wengi wamejadili suala la mkataba wa uendeshaji wa bandari, jambo ambalo linaonyesha jinsi Rais Samia Suluhu Hassan amejenga mazingira bora na salama ya Watanzania kutoa maoni yao.


“Kama kuna watu walikuwa na mashaka na uzalendo, na uimara, na uthabiti wa Bunge hili, bila shaka leo tumethibitisha hili Bubnge ni imara sana. Waheshimiwa wabunge mmethibitisha kwamba nyinyi ni wazalendo, nyinyi ni imara, nyinyi ni thabiti na hampo hapa kwa bahati mbaya, mko kulinda maslahi ya nchi yetu,” amesema na kuongeza;

“Naomba kuchukua nafasi hii kumpongeza Rais Samia, kama kulikuwa na watu wana mashaka na uzalendo wake, uimara wake, uthabiti wake, bila shaka katika jambo hili tumethibitisha na Rais amethibitisha ni mzalendo, ni imara, ni thabiti, anayestahili kuendelea kuaminiwa kuliongoza taifa hili.”

Amewaomba wabunge wapitishe kwa kishindo makubaliano hayo ili kupeleka salamu na Watanzania wote wawaunge mkono ili kuwaadhibu wale wanaotaka kuligawa Taifa hili, wasirudie tena.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments