RAIS SAMIA AWATAKA YANGA WABORESHE MASLAHI YA WACHEZAJI, WAMALIZE MZOZO NA FEI TOTO MARA MOJA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi na wadhamini wa Young Africans SC kuwaboreshea wachezaji maslahi yao sanjari na kuwakumbusha kukaa meza moja kufanya mazungumzo na Kiungo Feisal Salum (Feitoto).

Rais Samia amesema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akiipongeza Klabu hiyo licha ya kukosa Kombe la Kombe la Shirikisho barani (CAF CC), Kikanuni. Rais Samia amesema: “Kwa mafanikio haya, viongozi na mashabiki wa Yanga SC, hakikisheni mnaboresha maslahi ya wachezaji wenu ili wachezaji hawa walete mafanikio zaidi.”

“Nawaombeni kukaa chini na kufanya mazungumzo na Mchezaji Feisal Salum (Feitoto) ili muweze kulimaliza hili suala, na mimi nitakuwa tayari kuwakaribisha nyumbani endapo mtayamaliza haya yanayoendelea kwa sasa,” ameeleza Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesema Serikali itakaa chini kuangalia vizuri ombi la Yanga SC kutaka kupewa eneo kubwa katika eneo la Jangwani jijini Dar es Salaam ili waweze kujenga uwanja mkubwa wa kisasa na kuchochea kuandaa Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027, mashindano yanayotarajiwa kuandaliwa na nchi Tatu za Afrika Mashariki, Tanzania, Kenye na Uganda.

Vile vile, Mhe. Samia amewataka mashabiki na wadau wa Soka nchini kuweka pembeni utani wa jadi wakati timu za Tanzania zinapowakilisha nchi Kimataifa, Mhe. Samia amesema mashabiki na wadau hao wa soka wanapaswa kuwa kitu kimoja wakati timu hizo zinapowakilisha nchi katika mipaka ya Kimataifa.

“Tunataka utani wa jadi uwe ndani ya nchi pekee, lakini timu zetu zinapotoka nje ya mipaka yetu, Watanzania wote tunapaswa kuwa kitu kimoja ili tuwape moyo wale wanaopambana ili wafanye vizuri katika mashindano hayo.”

Yanga SC imealikwa Ikulu jijini Dar es Salaam na Rais Samia baada ya kuwa washindi wa pili wa Michuano ya CAF CC baada ya kufungwa Kikanuni kwa jumla ya mabao 2-2 na timu ya USM Alger ya Algeria katika michezo miwili iliyopigwa Mei 28 jijini Dar es Salaam na Juni 3, 2023 mjini Algers.



















































TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments