Rais Samia kufanya ziara Mwanza, kukagua daraja la JPM

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anaanza ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Mwanza leo Juni 12, 2023 ambapo pamoja na mambo kadhaa, atakagua miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa daraja JPM maarufu kama Kigongo-Busisi linalopita juu ya maji ya Ziwa Victoria.

Mkuu huyo wa nchi anatawasili jijini leo ambapo kesho Juni 13, 2023 atazindua tamasha la ngoma za asili za Jamii ya Kisukuma maaruu kama Bulabo litakalofanyika makumbusho ya Bujora Wilaya ya Magu.

Taarifa ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza inaonyesha kuwa Juni 14, Amiri Jeshi Mkuu huyo atatembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa daraja la JPM (Kigongo-Busisi) linaloongonisha Wilaya zaa Misungwi na Sengerema linalojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh716 bilioni.


Ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa Kilometa 3.2 ukiwa pia na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.66 ulianza Februari 25, 2020 na unatarajiwa kukamilika Februari 24, 2024.

Taarifa ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mwanza umesema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 75.

Utakaopokamilika, daraja la Kigongo-Busisi utapunguza muda wa kuvuka hadi dakika 5 kwa kutumia gari na dakika 15 kwa watembea kwa miguu kulinganisha na muda wa sasa wastani wa dakika 25 hadi 45 kwa kutumia kivuko.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amesema siku hiyo ya Juni 14, Rais Samia pia atatembelea Bandari ya Mwanza Kusini kukagua mradi wa ujenzi wa meli mpya ya Mv Mwanza ‘Hapa Kazi Tu’ unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh109 bilioni.

Utekelezaji wa mradi ujenzi wa meli ya Mv Mwanza ulioanza Januari, 2019 unatarajiwa kukamilika mwaka huu.

Meli hiyo itakayokuwa kubwa kuliko zote ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ina kimo cha ghorofa nne ikiwa na urefu wa mita 92.6, upana wa mita 17 na uzito wa tani 3, 500 huku ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1, 200, magari 20 na tani 400 ya mizigo.


Rais Samia atahitimisha ziara yake mkoani Mwanza Juni 15, 2023 kwa kukagua mradi wa ujenzi wa hotel ya kisasa jijini Mwanza unaotekelezwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments