Samia azipa angalizo NGOs masharti ya wafadhili

 Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa tahadhari kwa wamiliki wa taasisi zisizo za kiserikali na asasi za kiraia zinazotoa misaada nchini kuhakikisha wanazingatia mila, tamaduni na maadili ya Watanzania.

Samia ameyasema hayo leo Jumapili Juni 25, 2023 katika kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya kupinga matumizi na biashara ya dawa za kulevya duniani jijini Arusha alipokuwa akipita katika mabanda tofauti tofauti yanayotoa huduma kwa waraibu wa dawa za kulevya na kushughulikia biashara hiyo haramu.

“Ninataka niwaambie ninyi mashirika kuwa hao wafadhili ambao mnapokea fedha zao kwa ajili ya kuwasaidia vijana wetu kuna vijicondition (baadhi ya masharti) mnawekewa na hao wanaowapatia fedha, naomba niwaambie mbaki katika mstari kuhakikisha mnalinda mila na tamaduni za Watanzania,” amesema Rais Samia.


Kamishna wa huduma za sheria katika Mamlaka ya dawa za kulevya, Veronica Matikila amesema kitengo hicho kimesaidia kuboresha mashauri ya kesi zinazohusu dawa za kulevya na kwamba takwimu zinaonyesha kuanzia Aprili mwaka jana mpaka Mei mwaka huu jumla ya mashauri 6818 yamefanyiwa kazi.

“Mashauri 6,818  yameshughulikiwa kati ya hayo mashauri 900 Serikali imeshinda na 158 wananchi waliachiwa huru hii inaonyesha haki inatendeka. Mashauri zaidi ya 2,000 upelelezi unaendelea,” amesema Veronica.

Mwanasaikolojia kutoka kitengo cha mamlaka ya dawa za kulevya, Deogratius Mwamale amesema mpaka sasa vitengo vya tiba ya waraibu nchini (MAT) kuna kliniki 15 nchi nzima, nyumba za kuwahudumia waathirika (sober house) zipo 50  na mwaka wa fedha ujao mamlaka hiyo inatarajia kujenga ‘sober house’ mikoa ya Dodoma, Mwanza na Arusha kwa ajili ya kusaidia vijana hao ili nguvu kazi ya Taifa isizidi kupotea.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments