Recent-Post

‘Wanafunzi waruhusiwe kushiriki siasa vyuoni’

Zuio la wanafunzi kushiriki shughuli za siasa wakiwa shuleni, limeelezwa na wadau kuwa kikwazo cha ukuaji wa demokrasia.

Wadau hao wamependekeza yafanyike mabadiliko ya mfumo wa elimu ili kundi hilo lijengewe misingi ya demokrasia likiwa shuleni.

Licha ya zuio hilo, baadhi ya vyama vimekuwa na taasisi zao vyuoni, ikiwamo CCM yenye Mkoa wa vyuo vikuu na Chadema yenye Umoja wa wanafunzi wa vyuo vikuu (Chaso).

Hatua ya vyama kujiimarisha vyuoni iliwezesha kutengeneza wanasiasa mahiri, wakiwemo Halima Mdee, Zitto Kabwe, John Mnyika, Zainab Abdala, Kheri James, Hamis Kigwangala na wengineo.

Wakijadili Jumanne Juni 27, 2023 wakati wa mjadala kwenye kongamano la Kigoda cha Mwalimu Julius Nyerere cha Umajumuhi wa Afrika lilichofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wametaka elimu ya demokrasia itolewe kwa wanafunzi.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza alisema hakuna namna vijana wataweza kuwa hai kwenye masuala ya demokrasia wakati hawaandaliwi kufikia hatua hiyo.

“Unataka kijana ashiriki masuala ya kidemokrasia wakati shuleni, chuoni kuna marufuku ya kujihusisha na siasa, anawezeje kufikia hatua hiyo wakati haandaliwi na kujengewa misingi hiyo tangu mdogo?

“Tunataka vijana waliolelewa katika misingi ya kidemokrasia ni lazima wapewe nafasi ya kujifunza siasa kuanzia chini,” alisema.

Akizungumzia hilo, mwalimu wa somo na uraia na jiografia wa sekondari Alpha, Lugete Mussa alisema changamoto iliyopo ni walimu kutumia muda mwingi kutengeneza matokeo na kuwakaririsha wanafunzi waweze kufaulu mitihani badala ya kuwajengea uwezo wa kupata maarifa na weledi.


Lugete alisema udhaifu huo unaonekana hata kwenye vyuo vikuu kutokana na mfumo wa elimu kutowapa nguvu wanafunzi kutengeneza maarifa na kuwa wabunifu, akitolea mfano namna wahadhiri wanavyochangia kuwafanya wanafunzi kukariri na sio kuelewa kile anachojifunza.

“Imekuwa si ajabu kukuta mtoto ana kiwango kikubwa cha ufaulu kwenye masomo yake lakini hana maarifa ya kutosha na hawezi kukitetea kile alichonacho kichwani. “Jingine ninaloliona walimu tunafanya kazi kubwa kuwafurahisha wenye shule kwa kuhakikisha watoto wanafaulu na sio kuelewa kile wanachofundishwa,” alisema.

Awali akiwasilisha mada katika kigoda hicho, mshauri mwelekezi wa shirika la Hakielimu, Dk Wilberforce Meena alisema licha ya walimu kuwa na jukumu la kuwawezesha vijana kukuza umahiri wa demokrasia, mfumo wa shule hauwapi uhuru huo walimu.

Dk Meena alieleza kuwa kwa sasa msisitizo mkubwa katika mfumo wa shule ni wanafunzi wafanye mtihani na kufaulu kitu kinachowafanya walimu watumie muda mrefu katika eneo hilo na sio kuwajengea wanafunzi stadi za kidemokrasia.

“Walimu wanaendeshwa na sheria na miongozo mingi ambayo inawafanya watekeleze vitu ambavyo tayari vimeshaamuliwa na kwa sababu hiyo, wanashindwa kuwa na uhuru wa kuwajengea wanafunzi umahiri wa kidemokrasia.

“Ni lazima walimu wajengwe pia kuwa wataalamu wa demokrasia ili waweze kuwashinda wanafunzi wao kuiishi hiyo demokrasia, kinyume na hapo tusitegemee kuwaona vijana wengi wakishiriki haya masuala ya kidemokrasia,” alisema Dk Meena.

Akizungumza kwa simu na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa ngome ya vijana ya ACT Wazalendo, Abdul Nondo alikiri kwamba mfumo uliopo unawarudisha nyuma vijana kushiriki katika masuala ya kidemokrasia, ikiwemo siasa kwa hofu ya kuonekana wanatumika.


“Kuna vitu vingi vinavyowafanya vijana wasijihusishe na masuala haya ya demokrasia, ikiwemo hofu maana ukikosoa ujiandae kukamatwa na kufuatiliwa, ukosefu wa ajira ni sababu nyingine inayowafanya vijana wajiweke kando,” alisema.


Post a Comment

0 Comments