Kwenye fainali hiyo ya pili, Yanga iliingia huku ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 2-1 kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja Mkapa na ilihitaji ushindi wa 2-0 tu ili kutwaa ubingwa.
Kutokana na spidi yao ya kuliandama lango la USM Alger, Yanga ilipata bao moja la penalti lililofungwa na Djuma Shaban, baada ya mshambuliaji Kennedy Musonda kuangushwa eneo la hatari.
Bao hilo lilifanya jumla kuwe na mabao 2-2, lakini USM Alger ilichukua ubingwa kwa kigezo cha kushinda mabao mengi wakiwa ugenini.
Mfumo waibeba Yanga
Yanga kwenye mchezo huu iliingia kwa kucheza mfumo wa 3-4-3 ambao uliwafanya wapinzani wake wawe kwenye wakati mgumu kuwasogelea hasa kwenye kipindi cha kwanza.
Yanga nyuma ilichezesha mabeki wa kati wa tatu, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca na Dickson Job huku upande wa kiungo kukiwa na Salum Abubakari, Mudathir Yahya,Joyce Lomalisa na Djuma Shaban.
Shaban na Lomalisa wenyewe walikuwa wanatumika zaidi kwenye kupeleka mipira ya pembeni huku ikitokea wakipitwa na wapinzani basi mabeki wa kati wanamaliza shughuli mapema.
Upande wa ushambuliaji alisimama Fiston Mayele, Tuisila Kisinda na Kennedy Musonda.
Alger walikuwa na wakati mgumu kwani kuvuka eneo la katikati ya uwanja ilikuwa ni tabu na pindi Yanga wanaposhika mpira kupeleka mbele ilikuwa ni rahisi kutokana na wingi wao wa wachezaji.
Bao la mapema lawavuruga
Bao la mapema lililofungwa kipindi cha kwanza dakika ya 10 kwa mkwaju wa penalti ya Djuma Shaban baada ya Musonda kuangushwa, liliwaweka mchezoni zaidi Yanga na kuona tayari wameshawaweza Alger.
Alger kwenye kipindi cha kwanza walishindwa kuendana na presha ya Yanga na kujikuta wakiwa watumwa kwani wapinzani wao walikuwa na spidi ya kutosha ndani ya dakika 45.
Yanga ilikuwa na uwezo wa kufunga hata mabao mawili kwenye mchezo huu hasa kwenye kipindi cha kwanza lakini mambo hayakwenda vizuri na kufanya waende mapumziko wakiongoza bao moja.
Alger walitaka kubadilika kwenye dakika za kwanza kwenye kipindi cha pili kuhakikisha wanapata bao lakini ngoma ilikuwa ngumu kutokana na umakini wa mabeki wa kati.
Lomalisa katika ubora wake
Kwenye mchezo huu Nabi alimpumzisha Kibwana Shomari na kumpa nafasi mkongwe Joyce Lomalisa ambaye ana uzoefu na mechi kubwa kama hizi baada ya kucheza akiwa na timu tofauti tofauti.
Lomalisa alionyesha utulivu akicheza vizuri kwenye kuzuia zaidi hasa kipindi cha kwanza na kufanya mashambulizi ya kushtukiza langoni kwa Alger akitumia krosi za mbali.
Beki huyu alihakikisha nahodha wa Alger, hatembei na mipira na mara kwa mara alifanikiwa kwa kucheza mipira kwa kuingia chini kwenye miguu ya mchezaji huyo hadi akaonyeshewa kadi ya njano.
Hata alipotoka na nafasi yake kuingia Farid Mussa kwa ajili ya kupeleka mashambulizi mbele, Lomalisa tayari alishaonyesha uwezo wake wa kupiga krosi kati ya uwanja sambamba na kukaba wapinzani.
Waarabu waomba mpira uishe
Bao la mapema Yanga na namna ambavyo walikuwa wanacheza kwenye mchezo huu, waarabu waliona mambo yameshaanza kuwa magumu hivyo kwenye kipindi cha pili walikuwa wakitumia zaidi kujiangusha ili kupoteza muda.
Kocha Nassredine Nabi wa Yanga mara kwa mara alionekana kuzozana na waamuzi juu ya jambo hilo la wachezaji wa USM Alger kuanguka anguka ili kupoteza muda wa kucheza mechi hiyo.
Jambo lingine ambalo lilifanya mchezo upunguzwe presha ni kitendo cha mashabiki kutumia mafataki kuingia uwanjani na kutoa moshi kitendo ambacho kilifanya mechi isimame takribani mara mbili.
Mechi ilipokuwa inasimama kwa takribani dakika tano au nne pindi inapokuwa inarejea tayari inakuwa imetengeneza utulivu kwa wachezaji wa timu zote mbili tofauti na ilivyokuwa awali.
Mbinu ya kujiangusha angusha kwa waarabu ni ya muda mrefu kwani hata vizazi vya zamani navyo vimekuwa vikitumia sana kwa lengo la kuchelewesha muda hasa ambapo wanakuwa na matokeo mazuri.
Diarra, Mudathir usipime
Hakuna shaka kwamba kipa Diara Djigui amezidi kudhiirisha kwamba yeye ni miongoni mwa makipa bora kwenye Ligi Kuu Bara na hata kimataifa kwani penalti aliyocheza kwenye mchezo huu iliendelea kuwaweka mchezoni Yanga.
Nahodha wao Zidane Belaid mkwaju wake ulidakwa na Diarra na kama lingekuwa bao basi lingezidi kuwanyong'onyesha Yanga, lakini alivyodaka ndio iliwarejesha zaidi mchezoni.
Licha ya Diarra kucheza penalti hiyo bado aliendelea kuwa kwenye kiwango kizuri akiokoa michomo kadhaa ambayo ingeweza kuzaa bao kwa USM Alger, lakini hakuwa tayari kuona hilo linatokea.
Kipa huyu pia alikuwa anazungumza na mabeki wake mara kwa mara kwa lengo la kuhakikisha wanacheza kwa maelewano makubwa bila kuruhusu washambuliaji wa timu pinzani wanaingia kirahisi ndani ya boksi.
Upande wa Mudathir Yahya kwenye eneo la kati ya uwanja alikuwa na kazi ya kuhakikisha anakaba, lakini pia anamfanya Salum Aboubakar awe huru kuchezea mpira na kupiga pasi za mwisho.
Mudathir alikuwa anasafa huku na kule kuhakikisha viungo wa USM Alger hawawi huru kwenye kucheza mipira yao na kutokana na kukaba kwake mara kwa mara alionyeshewa kadi ya njano kwenye mchezo huu.
Mayele atulizwa
Mshambuliaji Fiston Mayele ambaye ana mabao saba kwenye kombe la Shirikisho, kwenye mchezo huu alifichwa kabisa na hakupewa nafasi kabisa ya kufanya anavyotaka na hilo ni kutokana na kujulikana kwake kwa sasa.
Mayele alikuwa anatembea na mabeki wawili hadi watatu na kumfanya mshambuliaji mwenzake Kennedy Musonda kuwa huru sana kwenye mchezo huu kwani hakuwa tishio.
Mshambuliaji huyu baada ya kuona anakabwa sana ilimlazimu kukimbia na kutoka kabisa karibu na goli kisha akawa anafata mipira kwenye eneo la kati au pembeni kisha akimbie nayo na kupiga mashuti.
Presha ya kufunga ambayo alikuwa nayo ilimfanya muda mwingine afanye maamuzi ya kupiga mashuti nje ya goli hata kama sehemu ambayo alikuwa na uwezo wa kupiga pasi kwa mwenzake na alijikuta akiikosesha timu nafasi nzuri ya kufunga.
Morrison, Aziz Ki wakosa utulivu
Mashabiki wengi waliona kuna ahueni kidogo walipoingia Benard Morrison na Stephen Aziz Ki kwenye mchezo huu kwani ni wazuri kwenye umiliki wa mpira na kupeleka mashambulizi langoni kwa timu pinzani.
Katika mchezo huu wa fainali ilikuwa tofauti kwa wawili hawa kwani mara kwa mara walikuwa wanapoteza mipira huku wakiwaacha midomo wazi benchi la ufundi na hata mashabiki.
Morrison ambaye amezoeleka kukera na kupenya kwa mabeki wa timu pinzani, kwenye mechi hii alikuwa mzito na hata kwenye sifa yake ya kuchonga kona nzuri bado alikuwa hafanyi hivyo.
Aziz Ki alikuwa akipoteza mipira kiasi cha kushindwa hata kuutuliza, jambo ambalo lilionekana alikuwa na presha kubwa ya mchezo kitu ambacho si kawaida kwake.
Rais Samia aiita Yanga Ikulu
Rais Samia Suluhu Hassan amekialika kikosi cha Yanga kwa chakula cha jioni Ikulu, Dar es Salaam, leo, kwa lengo kuipongeza kwa kufanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema jana kuwa Rais Samia ameipongeza Yanga kwa kucheza vizuri katika mchezo wa pili wa fainali juzi kwa kuwafunga wenyeji 1-0.
Msigwa alibainisha kuwa pamoja na kutotwaa ubingwa, Rais Samia anatambua kuwa Yanga imeipa heshima kubwa Tanzania na anawapongeza wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu hiyo, ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga na mashabiki wake walirejea nchini jana kwa ndege iliyotolewa na Rais Samia, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono timu hiyo iliyokuwa ikiiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
0 Comments