Kinana: Rais Samia msikivu, nchi imetulia

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahaman Kinana amesema Rais, Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa ndani ya miaka miwili kutokana na uongozi wake mzuri unaotokana na tulivu, usikivu, kupokea ushauri na kufanya uamuzi wa busara kwa manufaa ya Watanzania.

Kinana ameyasema hayo leo Jumapili Julai 23, 2023 wilayani Kondoa mkoani Dodoma katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mbunge wa Kondoa, Dk Ashatu Kijaji.

Lengo la mkutano huo lilikuwa kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kipindi cha miaka miwili na nusu chini ya uongozi wa Rais Samia.


“Kwa hali ilivyo na kwa hatua tuliyopiga tukienda hivi tunavyokwenda mpaka kufika 2025, mimi nina uhakika kila Mtanzania atakuwa na sababu ya kusema tuendelee na CCM, tuendelee na Rais Samia Suluhu Hassan. Hatutokuwa na sababu nyingine yoyote kwanza ni utamaduni wetu Chama cha Mapinduzi hatubadilishi uongozi katikati ya safari, ukitaka kubadilisha sababu itakuwa nini, hakuna.

“Lazima tumpe mtu nafasi yale aliyokusudia chini ya uongozi wa Chama chetu yatimie, ikifika 2025 tunakwenda na Rais Samia na Mwenyekiti wetu wa Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa amesema kila eneo, kila kata, kila mtaa kila jimbo yako ya kusemea mema, hatuahidi miujiza lakini tumeahidi na yale  tuliyoahidi, tumeyatekeleza kwa ufanisi mkubwa sana.

“Hatusemi haya kwa kujivuna bali kwa utekelezaji wa Ilani ya CCM,” amesema Kinana. Amesema CCM inaangalia pia wenzao wa nchi jirani wanakwendaje.

“Nchi yetu imetulia, ina amani, ina umoja, ina mshikamano, nchi ina malengo na ina mipango ambayo inatekelezwa na kila mtu ni shahidi, CCM itaendelea kuchaguliwa kwa sababu ina sera nzuri ina Ilani nzuri inayotekelezeka,” amesema Kinana.

Aidha, amesema; “kuna watu wamejaribu kutugawa kwa misingi ya udini, ukabila, ubara na visiwani wameshindwa.”


Amesema Bara la Afrika ziko nchi nyingi zimeajaribu kuungana na wanazifahamu ikiwemo Afrika Magharibi na nchi za Uarabuni zote zimesambaratika, lakini Tanzania muungano wake umeendelea kuwa imara na mwakani unafikisha miaka 60.

“Sababu ni misingi imara iliyojengwa na wasisi wa taifa letu hayati baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na marehemu Abeid Aman Karume, misingi yenyewe migumu na mnakumbuka katika vipindi mbalimbali muungano wetu umepitia kashikashi lakini tumeendelea kuwa imara,” amesema makamu mwenyekiti huyo.

Pamoja na hayo, Kinana amesema anaungana na wananchi wote pamoja na viongozi kumpongeza Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia kwa uongozi wake madhubuti.

“Wakati mwingine baadhi ya watu wanaona kama vile labda tunamsifu sana ndugu Rais, lakini hatumsifu kwa mambo tusiyo na uhakika, kama nilivyosema ushahidi upo,” amesema Kinana.

“Baadhi yenu mlifuatilia Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Dodoma mwezi wa 12, taarifa ilitolewa pale ikaelezea utekelezaji wa Ilani ya ya miaka miwili na miaka miwili hiyo wakati huo ilikuwa ni ya Rais Samia. Amefanya kazi kubwa sana, ili muweze kutekeleza kazi zenu vizuri lazima muwe na fedha za kutosha.

“Fedha hizo ni mapato ya ndani, mapato ya nje. Mapato ya ndani ya makusanyo yaliyokusanywa na serikali na taasisi zake mbalimbali miaka hii miwili kwa kila mwezi yako juu kuliko kipindi chochote katika historia ya nchi yetu, makusanyo yamefanikiwa bila mtu kusukumwa, bila kutishwa bila mtu kuwekwa mahabusu.

“Mapato kutoka nje yamekuja kwa sababu Rais na serikali yake chini ya uongozi wa CCM wamejenga mahusiano mazuri sana, dunia leo inatuamini zaidi, inatuheshimu na inatuthamini, nchi inakopesheka kuliko wakati wowote.”


Amesema hivi karibuni kulikuwa na mashirika mawili duniani yanayofanya tathimini ya hali ya uchumi na namna nchi inavyoweza kukopesheka, yote yametoa alama ya juu kwa Tanzania.

Amesema hiyo inamaanisha nchi ikitaka kutoa msaada kwa Tanzania, inaaminika.

Awali, akielezea utekelezaji wa Ilani Jimbo la Kondoa Vijijini, Dk Kijaji alimpongeza Rais Samia kwa kuitazama kwa karibu Wilaya ya Kondoa, kwa sababu katika kipindi cha miaka miwili na nusu, miradi ya maendeleo ya sekta mbalimbali  imepelekwa.

“Kwa kipekee niishukuru Serikali ya CCM chini ya uongozi thabiti wa Rais Samia kwa kutekeleza kwa vitendo na kwa ufanisi mkubwa Ilani yake ya 2020-2025. Wananchi wetu hapa jimboni  kila mmoja wetu anaona kwa macho miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa katika vijiji na vitongoji, hivyo basi naomba muendelee kukiamini Chama cha Mapinduzi,” amesema Dk Kijaji.

Wakati huo huo, wabunge na Wajumbe wa Halmashauri ya Taifa (NEC) ambao wamepata nafasi ya kuzungumza katika mkutano huo wameeleza kwa kina hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali katika kuboresha sekta ya bandari nchini huku wakitoa rai kwa wananchi kutosikiliza maneno ya upotoshaji yanayotolewa na baadhi ya watu ambao kimsingi wameishiwa hoja.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments