Machifu, viongozi wa dini wajitosa ushiriki wa Dk Tulia uchaguzi IPU

Machifu na viongozi wa dini Mkoa wa Mbeya wamesema ni wakati kwa  Watanzania kumuombea Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ili akashinde katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa urais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).


 Dk Tulia anakwenda kushiriki uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 2023, jijini Luanda, Nchini Angola huku akiwa anaungwa mkono na Wajumbe wa Jukwaa la Kibunge la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-PF).

Pia, tayari Maspika wa Mambunge ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekwoisha kutangaza kumuunga mkono.


Chifu Rocket Mwanshinga akizungumza katika uzinduzi wa Taasisi ya Suma Fyandomo jana Jumamosi Julai 8,023 Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, kwa niaba ya machifu wanalo jukumu kubwa la kumuombe kiongozi huyo wa Bunge kutokana na unyeti wa nafasi hiyo na kuliheshimisha Taifa la Tanzania.

“Nawaomba wananchi wa Mkoa wa Mbeya, kila mmoja kwa imani yake kufanya maombi kumuombe mwanetu Dk Tulia Ackson apite kwa kura za kishindo na kuendelea kupeperusha bendera ya Taifa la Tanzania katika mataifa mbalimbali duniani,” alisema Chifu Mwanshinga.

Alisema wakiwa kama machifu wanalojukumu la kuzungumza na kumuandaa Dk Tulia kuwa salama wakati wote ili aweze kuendelea kuwatumikia Watanzania hususan wananchi wa Jimbo la Mbeya mjini.

“Mungu ametupa nuru ya mwanetu Dk Tulia, tumemlea na kumkuza katika maadili mema na amekuwa kiungo kikubwa kwa wabunge wenzake katika Mkoa wa Mbeya na tunapoona mataifa mengine yakimuunga mkono tunafarijika sana,” amesema.

Naye Askofu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT), Dk Israel Mwakyolile alisema kama viongozi wa dini watafanya maombi rasmi kwa ajili ya kiongozi huyo ambaye amekuwa kiungo kikubwa kwa Taifa.

“Tuombe kila mtu kwa imani ya dini yake kufanya maombi kumuombe Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson Mungu amtangulie katika uchaguzi huo akapate kura za kishindo,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya, Mpokigwa Mwankuga alisema kama Wanambeya wanamuombea kila la kheri kiongozi huyo wa mhimili wa Bunge apate ushindi wa kishindo katika safari yake ya kuwania nafasi ya Urais wa Umoja wa Mabunge Duniani(IPU).

Naye Mkurugenzi wa Taasisi hiyo ambaye pia ni Mbunge Viti Maalum, Suma Fyandomo alisema lengo kubwa la kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kusaidia uwezeshwaji kwa watu wenye uhitaji wakiwepo wazee, wajane, wajasiriamali na makundi maalum katika Wilaya zote za Mkoa wa Mbeya.

Alisema hilo lilikuwa ni lengo lake la miaka mingi kutokana na kuona changamoto kwa wananchi ikiwepo hali duni ya uchumi, migogoro inayohusisha wanawake na wajane.

“Nilikuwa naumizwa sana kuona wanawake, wazee wakipata shida kiuchumi nikamuomba Mungu ambaye sasa kanifanikisha kutimiza azma yangu kwa kuweza kufungua taasisi hii ambayo itakuwa na mchango mkubwa kwa jamii kuwezeshwa kiuchumi,” alisema.

Fyandomo Taasisi yake pia imekabidhi vinu vya kukoboa na kusaga nafaka 12 vyenye thamani ya zaidi ya Sh64 milioni kwa ajili ya kuanzisha miradi ya wanawake sambamba na kutoa mashuka 50 na baiskeli kiti mwendo kwa ajili ya kusaidia watoto sita  wenye ulemavu.

Akizindua taasisi hiyo, Spika Tulia Ackson alisema ataunga mkono taasisi hiyo kupitia Taasisi yake ya Tulia Trust kuona jamii yenye uhitaji inafikiwa kupatiwa huduma wakiwepo wanawake, wazee na makundi maalum.

“Binafsi kupitia Taasisi ya Tulia Trust nitaungana na Taasisi ya Suma kuona pale penye uhitaji tunaongeza nguvu lakini pia nikutia moyo kwenye changamoto kubali maoni ya wananchi ili uweze kufikia malengo yako,” alisema.



TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments