Mbunge atumia Sh64 kusaidia jamii Mbeya

Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Mbeya, Suma Fyandomo ametoa vinu 12 vya kusaga na kukoboa nafaka vyenye thamani ya Sh64 milioni, kwa lengo la kuwasaidia wanawake kuanzisha miradi ya kiuchumi mkoani Mbeya.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa taasisi ya Suma Ikenda Fyandomo (SIF) leo, Jumamosi Julai 8, 2023 wilayani hapa, Fyandomo amesema ilikuwa ni ndoto yake ya muda mrefu kusaidia jamii.

“Nimeguswa kufanya haya mambo kutokana na kuwa mwanamke kiongozi ambaye naona changamoto za wazee, wanawake, wajane na kundi la watu maalum, na hii ilikuwa ni ndoto yangu kuisaidia jamii,” amesema.


Fyandomo amesema pia kupitia taasisi yake wameweza kutoa vitanda na mashuka kwa ajili ya wodi za wazazi kwenye vituo vya afya, taulo za kike kwa wanafunzi wa shule za sekondari na kutoa baiskeli sita za viti mwendo kwa watoto wenye ulemavu.

“Nashukuru sana kwa kuungwa mkono  na viongozi wa dini, Serikali na wadau katika siku hii muhimu ambayo nilikuwa nikimuomba Mungu anifanimishie, pia kuna mawaziri wameniunga mkono kwa kuchangia fedha kama sadaka yao wa watu wa Rungwe,” amesema.

Katika tukio jingine mbunge huyo amemkabidhi tuzo ya heshima Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, kama njia ya kutambua mchango wake katika mhimili huo wa dola.

Kwa upande wake Spika Tulia ambaye alikuwa mgeni rasmi ameshukuru jamii kwa kuunga mkono taasisi hiyo katika kuigusa jamii ya wenye mahitaji wakiwepo, wazee, wajane, walemavu na makundi mengine muhimu.

“Suma nichukue fursa hii kukupongeza kuzindua taasisi na kununua mashine 12 kwa ajili ya wanawake wa Mkoa wa Mbeya, kutoa vitanda na mashuka kwa ajili ya vituo vya afya jambo ambalo ni la heri sana katika jamii, ” amesema.

Dk Tulia amesema kuwa kupitia taasisi yake ya Tulia Trust, watashirikiana na taasisi SIF kuunga mkono na hivyo kuhakikisha jamii inafikiwa kwa kupata msaada ikiwepo uwezeshwaji wananchi kiuchumi.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema kama Serikali wataunga mkono uwepo wa taasisi hiyo kwa lengo la kuona jamii ya watu wa Mbeya inasaidika kupitia wabunge ambao wawakilishi wao bungeni.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments