Rais Samia atamani JKT ya kisasa zaidi

Amri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Samia Suluhu Hassan amesema ni matamanio yake kuona Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linakuwa la kisasa lenye kuwalea vijana katika uzalendo

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Julai 10,2023 wakati akihutubia kilele cha miaka 60 ya JKT katika uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Amesema vijana wanaotoka JKT wanapaswa kuwa wazalendo katika nchi yao na hata wanaobaki katika majeshi na vyombo vya ulinzi wawe watu wenye weledi wa kupigiwa mfano.

Rais amesema Serikali iko tayari kusimama na JKT na ikibidi kuwadhamini hata katika mikopo ili waweze kuimarisha vikosi vyao kwenye uzalishaji.

“Katika miradi mikubwa mmefanya vizuri sana ikiwemo ujenzi wa Ikulu ya Chamwino, sisi Serikali tutaendelea kuwaunga mkono na ikibidi mpate mikopo ili kuongeza nguvu ya uzalishaji tuko tayari kuwadhamini,” amesema Rais Samia.

Amesema vijana wanaopita JKT wanapaswa kubeba dhima ya uzalendo mioyoni mwao siyo katika midomo kwani jeshi linawafanya vijana kuwa wamoja na wenye kuithamini nchi yao katika kuonyesha uzalendo.

Kuhusu JKT ametaka waendelee na malengo yao ya kupunguza umasikini na utegemezi kwani ndiyo malengo makuu na kwamba Serikali itaendelea kuongeza nguvu ya kuwa na idadi kubwa ya vijana wanaopitia mafunzo hayo kuliko idadi ya sasa.

Kwa mujibu wa taarifa, idadi ya vijana waliokwenda JKT kwa mujibu wa sheria ni 52,000 ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka 30,000 walioitwa mwaka jana baada ya kumaliza kidato cha sita.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments