Waliofariki ajali ya Hiace kugongana na lori watambuliwa

Watu wa watano kati ya sita waliofariki dunia katika ajali ya basi dogo la abiria maarufu kama Hiace kugongana uso kwa uso na lori eneo la Mzibira Kata ya Uyovu Wilaya ya Bukombe mkoani Geita wametambulika.

Mganga Mkuu Wilaya ya Bukombe, Dk Deograsia Mkapa amewataja waliofariki dunia katika ajali hiyo iliyotokea Saa 12:07 alfajiri ya Julai 13, 2023 kuwa ni Habib Abeid (27) aliyekuwa dereva wa Haice na kondakta wake Aziz Omari (25).

Wengine waliotambulika ni mkusanya ushuru katika stendi ya mabasi Uyovu, Daniel James (27), Innocent John (25) na Magigi Shitabu (60) ambaye ni mfanyabiashara mjini Ushirombo huku maiti ya mtu mwingine aliyefariki katika ajali hiyo bado haijatambuliwa.


Dk Mkapa amewataja majeruhi wawili wa ajali hiyo kuwa ni Jackson Wizeye Joseph (38) na Wilson Daniel (49), wote wakazi wa Ngara mkoani Kagera.

Majeruhi hao awali walikimbizwa katika Hosipitali ya Uyovu kabla ya kupewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Geita kwa matibabu zaidi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari dogo la abiria kusinzia wakati gari likiwa kwenye mwendo kasi.

Gari la abiria iliyohusika katika ajali hiyo ilikuwa inatokea mjini Kahama kwenda eneo la Nyakanazi Wilaya ya Biharamulo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments