Bajaji Arusha wanuna kupangiwa vituo vipya

Madereva wa pikipiki za matairi matatu maarufu kwa jina la bajaji ndani ya jiji la Arusha wamegomea vituo vipya vilivyoainishwa na Mamlaka ya Usafiri Ardhini (LATRA) wakidai kuwa havijazingatia hoja zao walizozitoa kwenye vikao vya kamati walizokaa.

Upangaji wa bajaji hizo umekuja baada ya kutokea mgogoro baina yao na madereva daladala, uliosababisha kutokea mgomo wa siku mbini katika jiji hilo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi leo Agosti 17 mwaka huu, Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva Bajaji jiji la Arusha, Shafii Ndalo amesema kuwa vituo walizopangiwa hazina uhalisia wa biashara wala kutatua migogoro wao baina ya daladala bali zinalenga kuwakomoa.


Amesema kuwa awali Julai 3, baada ya mgomo wa daladala, walitoa maoni katika kamati iliyoundwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa, wakitaka kupangiwa vituo vya masoko, hospitali zote na binafsi, mahotelini na ofisi za umma ili kuondoa mgogoro huo.

"Sisi tuliitwa kikao na hoja kubwa ya daladala ilikuwa kuwaingilia kwenye ruti zao, hivyo tulikubali kuondoka na tukaomba bajaji zilizopo zipangwe kutoa huduma katika vituo vyenye muingiliano wa watu na uzuri wenzetu hawapiti huko.

"Nashangaa kwenye utekelezaji tunakwenda kupangwa maeneo yasiyo na watu kabisa mfano Lengijaphe, Nelson Mandela, Chekereni na kwingineko, huku ni kutukomoa maana hakuna mtu atakwenda kukaa njia panda ya kuelekea mashambani," amesema.

Naye dereva wa bajaji Mustapha Lewis amesema kuwa wanaiomba Serikali iangalie upya suala hilo, kwani inaweza kuleta hatari zaidi miongoni mwao kwani hawako tayari kuhamia pembezoni mwa mji wakati hakuna miundombinu inayoruhusu kufanya biashara huko.

"Mimi siko tayari kuacha roho ya kiuchumi mjini nikahamie mashambani, wakati awali Serikali yenyewe imetupa mikopo ya hizi bajaji halafu leo ituwekee mazingira magumu ya kurejesha.


“Kikubwa wao wasambaze miundombinu nje ya mji ikiwemo kusambaza ofisi zao za umma ziwe mbali mbali ili tuwafuate lakini wao wenyewe wamebanana mjini kati kwenye kata moja sisi hatuwezi kusambaa," amesema.

Awali ofisa mfawidhi wa Latra Mkoa wa Arusha, Joseph Michael amesema kuwa kwa mujibu wa uhakiki wa Bajaji hai zenye lesseni ni 749 na wamekwisha kupanga katika vituo 38 ambazo leo wanatarajia kuzisomea kwa ajili ya kuhamia.

"Tumezingatia uhai wa lesseni na mahali alipokuwa mtu awali hivyo kila kituo kina Bajaji zisizopungua tano wala kuzidi 30 hivyo baada ya kusomewa kila mtu atatakiwa kuhamia eneo lake la kazi," amesema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments