Recent-Post

CCM yawajia juu watendaji wazembe

Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Tanga kimekemea uzembe wa baadhi ya watumishi wa umma katika usimamiaji wa miradi ya umma mkoani hapa hali inayokwamisha utekelezaji wa miradi kwa wakati.

Kauli hiyo ya CCM ni kufuatia kusuasua kwa ujenzi wa kituo cha afya Mnyuzi na Kerege ambavyo vilitegewa Sh500 milioni kila moja.

Karipio hilo la CCM limetolewa na Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Tanga Rajab Abdallah wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM na kukiimarisha chama hicho ngazi zote katika mkoa huo pamoja na kusikiliza kero za wananchi.


Taarifa iliyosomwa na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mariam Cheche mbele ya mwenyekiti huyo na wajumbe wengine wa chama na Serikali ilisema vituo hivyo vyote viwili vilitakiwa kukamilika tangu mwaka jana kama maelekezo ya mradi yalivyoelekeza.

 "Leo katika ziara yetu tumekagua vituo viwili vya afya lakini vituo vyote tumekuta matatizo yanafanana hii haiwezekani Rais anahangaika kutafuta fedha kwa ajili ya kutatua changamoto za wananchi halafu fedha zinakuja lakini hapa Korogwe  majengo hayajamalizika kwakweli ni kitu chakusikitisha," amesema.

Mwenyekiti huyo amesema vituo hivyo vingekamilika kwa wakati vingewapunguzia  adha  wakazi wa maeneo hayo ambao wanatembea umbali mrefu wa kilometa zaidi ya 40 ili kufuata huduma zilizopo kwenye kituo cha afya korogwe.

Mwekiti huyo ametumia fursa hiyo kumuagiza mkuu wa wilaya hiyo na viongozi wengine kuhakikisha wanasimamia na kupitia nyaraka zote kisha wapeleke taarifa hiyo kwenye ofisi ya chama mkoa wa Tanga.

Rajabu Ameeleza kuwa Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya vituo vya afya lakini hapa mmeshindwa kukamilisha kwa wakati huku wananchi wakiitaji huduma hii ambayo ni muhimu kwao.


Mradi huu ulikuwa ukamilike ndani ya miezi minne lakini hadi sasa bado haujakamilika hamjui kama mnamchonganisha Rais Samia Suluhu Hassan na wananchi, hamuoni kama mnawachonganisha wabunge na wananchi wao lakini pia mnakichonganisha chama na wananchi,"amesema mwenyekiti huyo.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Korogwe vijijini Halfan Magani alisema walianza utekelezaji wa mradi huo mwaka wa fedha uliopita na kwamba sababu zilizopelekea kutokamilika kwa mradi huo kuwa ni changamoto za kimanunuzi  na kwamba mradi huo unatekelezwa kupitia ‘force account’.

"Sisi ngazi ya halmashauri kupitia kamati ambazo zipo kijijini wanakaa kwa ajili ya kuagiza vifaa kisha vinapelekwa kwenye idara ya manunuzi ndiyo wanakwenda kuvinunua wanaleta fundi anaendelea na utekelezaji," amesema mkurugenzi huyo na kuongeza kuwa mtu aliyekuwa anaongoza Idara ya manunuzi alikuwa na changamoto lakini hatua zimeshachukuliwa.

Mkurugenzi alieleza kuwa kwa upande wa kituo cha afya wanatekeleza kupitia Mkandarasi nakwamba mkandarasi huyo anasuasua kutekeleza mradi huo akidai mvua inanyesha hivyo wanashindwa kufikisha vifaa kwenye eneo la mradi.

Hata hivyo Mbunge wa Jimbo Hilo Timotheo Mzava alikiri kuwepo kwa changamoto katika mradi huo.

Post a Comment

0 Comments