Dk Dugange atinga bungeni, amshukuru mke wake

 Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Dk Festo Dugange ametumia sekundi 62 kutoa shukrani kwa Mungu, Rais, viongozi wa Bunge na Serikali pamoja na wananchi wa jimbo lake la Wanging'ombe.

Dugange ameingia bungeni leo Jumanne Agosti 29, 2023 kwa mara ya kwanza tangu alipojibu maswali Aprili 27, 2023 na baadye alipata ajali iliyokuwa na taarifa za utata.

Ajali ya kiongozi huyo ilihusishwa na kifo cha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambaye alizikwa Wilaya ya Iramba mkoani Singida huku familia ya binti huyo ikikafanua kuhusisha ajali hiyo na kifo cha binti yao.

Leo Jumanne Dk Dugange aliingia bungeni na kuitwa kwa ajili ya kujibu maswali ya wabunge akianza na swali namba mbili kwa siku ya leo.

Baada ya kuitwa mbele, wabunge walianza kumpigia makofi na kugonga meza ishara ya kumpongeza kwa kurejea kwake.

Naibu Waziri huyo alichukua muda mrefu akitaja orodha ya anaowashukuru akiwemo mke wake aliyemtaja kwa jina la Alafiza Moses Dugange.

Dk Dugange mapema leo amejibu maswali ya msingi matatu ikiwamo maswali ya nyongeza saba na hata alipomaliza aliendelea kushangiliwa.

Kwa mara ya kwanza Dk Dugange alionekana hadharani siku ya mashujaa katika viwanja vipya eneo la Mtumba jijini Dodoma ambako Rais alikuwa mgeni rasmi kwenye shehere hizo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments