Kawaida alia kuondolewa mikopo ya halmashauri kwa vijana

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Mohamed Ali Kawaida ameitaka Serikali Kuu na Mkoa wa Dar es Salaamu kutekeleza mambo manne ikiwemo kuharakisha mchakato wa kurejea upya mikopo ya asilimia 10 iliyositishwa Aprili mwaka huu.

Mambo mengine ni kuhakikisha inamaliza changamoto ya kamatakamata ya vijana wa bodaboda, vijana wafanyabiashara wasipigwe bali wapangiwe utaratibu wa kufanya shughuli zao pasipo usumbufu na kupewa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kawaida ameeleza hayo leo Jumapili Agosti 27, 2023 akihutubia katika mkutano wa hadhara wa UVCCM uliofanyika katika uwanja wa Zakhiem Mbagala wilayani Temeke. Mkutano huo ulikuwa wa majumuisho baada ya jumuiya hiyo kufanya ziara katika wilaya tano za Mkoa wa Dar es Salaam.

Katika maelezo yake, Kawaida amesema anatambua wizara husika (Ofisi ya Rais Tamisemi), ndio yenye jukumu la kusimamia suala hilo, lakini ameitaka kuharakisha mchakato huo ili mikopo itolewe na vijana waipate pasipo upendeleo hasa kwa walengwa mahususi.

Aprili 13, mwaka huu Serikali ilisitisha mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri hadi hapo utaratibu mwingine utakapoelekezwa. Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akihitimisha hoja yake ya makadiri  ya maombi na matumizi ya fedha kwa mwaka 2023/24

Fedha za halmashauri asilimia 10 hutolewa kwa mgawanyo wa makundi matatu ambayo ni wanawake asilimia nne na vijana asilimia nne huku asilimia mbili ikiwa imetengwa kwa ajili ya kuwakopesha wenye ulemavu.

"Ikianza kutoka basi itolewe bila upendeleo, bali wapewe vijana na watu wenye utayari sio kwa upendeleo.Lakini wanaotoa wahakikishe wanatoa elimu kwa wahusika kuhusu umuhimu wa mikopo hii.

"Naomba Serikali iharakishe mchakato huu,lakini vijana wenzagu mnaopewa mikopo hakikisheni mnarejesha kwa wakati ili wengine wapate," amesema Kawaida aliyeambatana na wajumbe wa baraza kuu la UVCCM katika mkutano huo.

Mbali na hilo, ameitaka Serikali ya mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha inamaliza changamoto ya kamata kamata inayofanywa na polisi dhidi ya vijana sambamba na kutaka kuhakikiisha vijana wanapangwa katika maeneo bora ya kufanya biashara zao.

Kwa mujibu wa Kawaida alisema lengo la ziara hiyo iliyoanzia Mjini Unguja ni kuimarisha uhai wa CCM na jumuiya hiyo, kuangalia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/25 na kusikiliza changamoto za vijana na wananchi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments