Miaka ya nyuma habari za kifo cha mtu iliweza kuchukua miezi au hata miaka kuwafikia wenzake waliokuwa naye shuleni, lakini sasa kutokana na mapinduzi ya teknolojia wanapata taarifa ndani ya muda mfupi.
Hali hii ni kutokana na kuwapo mitandao ya kijamii inayowakutanisha watu kidijitali, hivyo taarifa kusambaa kwa kasi na kuwafikia wengi.
Sasa watu wengi wapo kwenye makundi mbalimbali ya mitandao ya kijamii kama WhatsApp, Facebook, Telegram, Wechat na mingineyo. Katika kundi husika wanachama ni watu wenye maslahi sawa katika jambo fulani.
Yaweza kuwa ni kundi la wafanyakazi wa ofisi fulani, marafiki wa shule, ndugu nakadhalika, siku hizi ukitokea msiba michango huanzishwa katika jukwaa hilo na watu huanza kuchangia na wengine kutoa ahadi.
Huo ni utaratibu mzuri wa kijamii, ni rahisi kwa watu wenye kipato cha uhakika, lakini ni mzigo mzito kwa wasionacho.
Utafiti wa hivi karibuni wa FinScope 2023, unaonyesha watu wenye kipato cha chini au akiba isiyotosheleza mara nyingi hulazimika kupata mikopo ili kuchangia michango inayoendeshwa katika majukwaa ambayo ni wanachama.
Kilichobainishwa katika utafiti huo ni kuwa asilimia 49 ya washiriki waliopata mikopo ya dharura kutoka kwenye vikundi vya kifedha vya kijamii walifanya hivyo ili kuchangia rambirambi katika makundi yao.
Ingawa awali vikundi vya mikopo vya kijamii vilitambulika kama huduma za kifedha zisizo rasmi, sasa vinatajwa kama huduma rasmi za kifedha zisizo za kibenki.
Miriam Msuya, mkazi wa Tegeta, Dar es Salaam, anaelezea uzoefu wake kuhusu shinikizo la fedha lililosababishwa na michango ya mazishi.
“Kwa sasa mchango wa rambirambi hauwezi kuepuka, orodha ya wachangiaji inawekwa na kwa kuwa wananchi wa kipato cha chini ni waathirika kila wakati maafa hutokea, masuala ya kifedha yanakuwa changamoto kwa hivyo msaada kutoka kwa familia, jamaa na marafiki ni muhimu," anasema.
Anaeleza zaidi jinsi urahisi wa kupata na kumudu mikopo inayotolewa na vikundi hivi imemsaidia yeye na wengine kukabiliana na changamoto za dharura za kifedha zinazosababishwa na michango ya rambirambi.
Hata hivyo, kwa baadhi ya wanachama shinikizo la kuchangia rambirambi limesababisha kulimbikiza madeni, kwani baadhi ya makundi huwaorodhesha walioshindwa kuchangia rambirambi mara kadhaa.
“Baadhi ya wanavikundi wanajikuta wana madeni mengi kwa sababu mikopo hailipiki na shinikizo ni kubwa, kuna baadhi ya vikundi ukiwa hujachangia maafa matano unawekwa kwenye orodha ya watu ambao hawatakiwi kuchangia,” anaeleza.
Utafiti wa FinScope Tanzania 2023 unaonyesha kuongezeka kwa matumizi ya huduma rasmi za kifedha, huku huduma za fedha kwa njia ya simu zikichangia asilimia 72, ikifuatiwa na huduma za benki asilimia 22 na vikundi vya fedha vya kijamii vinachangia asilimia 12.
Kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za kifedha kwa njia ya simu na matumizi ya huduma za fedha kwa njia ya simu kumerahisisha michango ya rambirambi kupitia makundi ya mitandao ya kijamii.
Walter Fadhili, mkazi wa Kiluvya, anaelezea uzoefu wake juu ya changamoto ya kifedha inayotokana na kutakiwa kutoa mchango wa rambirambi.
“Kifo hutokea wakati mtu hana akiba, hivyo ili ueleweke katika jamii, unajikuta unakopa angalau Sh50,000 kutimiza hitaji hilo, kuna wakati nachukua hata mikopo yenye riba kubwa ili nichangie, umaskini utaendelea kuwa sehemu ya maisha ya baadhi ya watu ambao wana kipato kidogo,” anasema.
Rehema Mohammed, mfanyabiashara mdogo huko Mbezi Luis Dar es Salaam anasema ameshuhudia wenzake wakikimbilia mikopo ya vikundi vya kijamii ili kulipa michango ya mazishi.
“Binafsi sijawahi kuchukua mkopo katika kikundi cha jamii ili kulipia michango ya mazishi, lakini nimeona wenzangu wakifanya hivyo,” anasema.
Wataalamu wa masuala ya ustawi wa jamii na uchumi wameeleza kuwa utandawazi na matarajio ya jamii ni mambo yanayochangia pakubwa kupanda kwa gharama za mazishi.
Watu sasa wanalazimika kutumia gharama kubwa kwenye mazishi, ikiwa ni pamoja na gharama za usafiri na sare maalumu. Matokeo yake, watu wengi wanageukia mikopo ya haraka ili kukidhi mahitaji haya ya kifedha.
Teofrida Mbilinyo, mtaalamu wa ustawi wa jamii, anaamini kuwa mzunguko wa fedha umekuwa mdogo, hivyo kuwasukuma watu kuelekea kwenye vikundi vya kijamii ambapo wanaweza kupata mikopo haraka ili kushiriki mazishi kwa namna wanavyopenda.
Zaidi ya hayo, utandawazi umechangia kuongezeka kwa gharama zinazohusiana na mazishi.
Mbilinyo anaeleza, "Msibani, mbali na kulipa michango, utalazimika kuvaa sare na kusafiri kwa sababu aliyefiwa au aliyefariki alikuwa mtu wa karibu. Hizi zote ni gharama, ukiwa huna akiba, lazima utafute njia mbadala ya kupata pesa haraka."
Hata hivyo, kukosekana kwa ujuzi sahihi wa masuala ya fedha kumesababisha wakopaji kushindwa kurejesha mikopo yenye riba kubwa, hivyo kusababisha hasara ya mali zao na matatizo ya kifedha.
Anasema kuna haja ya kutoa zaidi elimu ya fedha katika ngazi ya chini ili kuhimiza uwekaji akiba binafsi na uwekezaji.
Ofisa mwingine wa ustawi wa jamii, Jasmine Mallya anasema shinikizo la kijamii la kuthibitisha na kukubalika katika jumuiya ya kimtandao ndiyo sababu ya kulemewa na mizigo ya ziada ya kifedha kwa watu binafsi na familia.
“Elimu ya fedha lazima itolewe kwa jamii katika ngazi ya chini ili watu waondokane na njia za jadi za matumizi bila kuweka akiba.
Habari hii kwa mara ya kwanza ilichapishwa na gazeti dada la The Citizen Julai 29, 2023.
0 Comments