MSTAAFU PSSSF AMSHUKURU RAIS SAMIA KWA KUWALIPA MAFAO NA PENSHENI KWA WAKATI

 MSTAAFU wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kutoka wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, Bi. Monica Kamoza, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwajali Wastaafu na Wazee kwa kuwalipa pensheni na mafao kwa wakati.


Bi. Kamoza ametoa shukrani hizo Jumamosi Agosti 5, 2023 wakati akikabidhi zawadi ya boga kubwa kwa watumishi wa PSSSF kufuatia kile alichoeleza ni kufurahishwa na huduma nzuri anazopata kutoka PSSSF

“Ninamshukuru sana Mhe. Rais kwa upendo wake, anatujali sisi Wastaafu na Wazee, haya yote tunayofurahia ya kupata huduma bora yanatokana na uongozi wake mzuri.” Alisema

Bi Kamoza ambaye alikuwa mfanyakazi katika hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Kyela akiwa kama mtaalamu wa afya ya macho, alistaafu Desemba 26, 2021 na kilichompeleka kwenye banda la PSSSF ni kupata huduma zinazohusiana na taarifa zake za ustaafu.

“Nimefurahishwa na huduma safi na za haraka nilizopewa kwenye banda la PSSSF, kilichonileta hapa ni kupata taarifa yangu ya malipo ya mkupuo ili nijue kama kulikuwa na mapunjo au la, nimepewa taarifa na ufafanuzi wa kina na hakukuwa na mapunjo yoyote.” Alifafanua Bi. Kamoza.

Mstaafu huyo alisema, ukiacha huduma aliyopewa kwenye banda hilo, jambo lingine lililomfurahisha hata wakati anastaafu alipata malipo yake ya mkupuo ndani ya mwezi mmoja na hata malipo ya pensheni ya kila mwezi hayajawahi kuchelewa.

“Mwezi uliopita (Julai) nimepokea malipo yangu ya pensheni tarehe 21, mwezi wa sita tarehe 24, kwa kweli nawapongeza sana kwa huduma zenu bora na nzuri.” Alipongeza.

Akizungumza baada ya kupokea zawadi hiyo kwa niaba ya wafanyakazi wa Mfuko wanaotoa huduma kwenye banda la PSSSF, Mhasibu Mkuu wa PSSSF, Bi. Grace Kabyemela, alimshukuru Bi. Kamoza kwa zawadi hiyo kwa wafanyakazi wa PSSSF.

“Zawadi hii ina maana kubwa sana kwetu, inaonyesha kutambua ubora wa huduma tunazotoa kwa wanachama na wastaafu wa Mfuko na tunachoahidi ni kuendelea kutoa huduma bora na za viwango.” Alisema.

Huduma zinazotoelwa kwenye banda la PSSSF ni kama zile zinazotolewa kwenye ofisi za Mfuko huo zilizoenea kote nchini.

Mwanachama wa PSSSF anapofika ataweza kupata taarifa za uanachama wake, taarifa za michango, taarifa za mafao, taarifa za uwekezaji, mstaafu ataweza kujihakiki na kupata elimu ya hifadhi ya jamii kwa ujumla.

Mhasibu Mkuu wa PSSSF, Bi. Grace Kabyemela, akipokea zawadi ya boga kubwa kutoka kwa Mstaafu Bi. Monica Kamoza

Mfanyakazi wa PSSSF, Bi. Zainab Mjungu (kushoto) akimkabidhi mstaafu wa PSSSF, Bi. Monica Kazola, taarifa ya malipo ya mkupuo alipofika kwenye banda la PSSSF kupata huduma.
Mstaafu wa PSSSF, Bw. Jimmy Nyamoga, akijihakiki kwenye banda la PSSF Agosti 5, 2023. Kushoto ni Bi.Zinab Mjungu.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali Laban Thomas (kushoto) akimsikiliza Afisa Uhusiano Mkuu PSSSF, Bw. Abdul Njaidi, alipotembelea banda la Mfuko huo Agosti 5, 2023.

Afisa Matekelezo Mwandamizi PSSSF, Bi. Winfrida Siriaki Jory (kushoto) akimsikilzia mwanachama wa Mfuko huo, akiyefika kupata elimu kuhusu uanachama wake.

Afisa wa PSSSF, Bi. Saluna Aziz Ally (kulia) akimuelekeza mwanachama wa Mfuko huo jinsi ya kutumia huduma za Mfuko kupitia PSSSF Kiganjani.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments